Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa shule ya Sekondari Kigoma ilihali wakala wa Majengo TBA  wanaojenga shule hiyo walishapatiwa fedha  za awali kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo kiasi cha asilimia 30 na kuwa malipo ya fedha hizo yalishafanyika tangu mwezi machi mwaka Jana.

Waziri Ndalichako amesema shule ya sekondari Kigoma ni miongoni mwa Shule Kongwe na tayari Serikali imekwishatoa fedha za kutosha ambapo ukarabati wa shule ulitarajiwa kukamilika mapema Mwezi Septemba, 2017  ili shule zitakapofunguliwa Januari  8, 2018 ukarabati uwe umekamilika na wanafunzi waweze kutumia miundombinu hiyo.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo akiwa mkoani Kigoma kwenye ziara ya kikazi ya kukagua ujenzi na ukarabati wa shule mbalimbali unaotekelezwa na Wizara yake kupitia Programu maalumu ya Lipa kulingana na matokeo na kusisitiza kuwa wakala wa majengo lazima wachukuliwe hatua kwa kuchelewesha ujenzi wa shule hiyo .

Kufuatia kusuasusa kwa ukarabati wa shule hiyo ya sekondari Kigoma, Mkuu wa mkoa wa kigoma Brigadia Jenerali mstaafu Emmanuel Magaga  ameamuru kukamatwa na kuwekwa ndani kwa meneja wa Wakala wa majengo wa TBA wa mkoa wa Kigoma Mgala Mashaka  ili uchunguzi ufanyike dhidi yake kutokana na kutuhumiwa kujihusisha na miradi binafsi, pamoja na kuhusishwa na vitendo vya rushwa.


Akiwa mkoani Kigoma Waziri Ndalichako pia alikagua vifaa vya maabara ambavyo tayari vimepokelewa kwenye shule mbalimbali za mkoa huo.

Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA
5/1/2018
Share To:

msumbanews

Post A Comment: