KAMANDA WA POLISI MKOA WA GEITA, MPONJOLI LOTSON.


MJANE mkazi wa kijiji cha Kamhanga, wilaya na mkoa wa Geita amefariki dunia baada ya kukatwakatwa na panga kichwani na mwanaye usiku na kisha mtoto huyo kutoroka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Lotson alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo, jana na kumtaja marehemu kuwa ni Kabula Karume (73).

Mtuhumiwa anayedaiwa kutoroka baada ya kutekeleza  ukatili huo ni Dotto Lukenze na chanzo cha mauaji hayo bado hakijajulikana na upelelezi unaendelea.

Kamanda Mponjoli alisema kuwa taarifa za awali za kikachero zinaonyesha mtuhumiwa ana rekodi ya kuwahi kutuhumiwa kwa mauaji katika matukio mengine na uhalifu mbalimbali.

Habari kutoka eneo la tukio zinadai kuwa kabla ya mauaji hayo, mtuhumiwa ambaye ni mtoto wa marehemu alikuwa akimshinikiza mama yake kuuza mali zikiwamo ng'ombe na mashamba, hatua ilikuwa ikipingwa na marehemu.

Mponjoli alisema siku ya mauaji Januari 16, mwaka huu saa tatu usiku marehemu alikuwa akiota moto na watoto wake wengine na ghafla ndipo mtuhumiwa alipotokea na kuanza kumshambulia.

Alisema katika kutekeleza mauaji hayo mtuhumiwa alitumia kitu chenye ncha kali kumkatakata kichwani marehemu huku waliokuwapo wakijaribu kupiga kelele za kuomba msaada bila mafanikio.

Watu hao ndiyo walimtambua mtuhumiwa kabla hajakimbia, alisema Mponjoli
Share To:

msumbanews

Post A Comment: