Hata kabla hajaanza kibarua cha kuinoa Simba, imebainika Kocha Mkuu mpya wa klabu hiyo Pierre Lechantre, amewanyoosha vibaya makocha wenzake waliopo klabu kubwa za Yanga na Azam.
Unaambiwa Mfaransa huyo kwa dakika atakuwa anavuta kiasi cha Sh42,000 ambacho ni sawa na Sh700 kwa kila sekunde inayogonga kwenye mshale wa saa.
Ndio, kwa mujibu wa mmoja wa viongozi wa Simba, Mfaransa huyo atalipwa kiasi kisichopungua Sh30 milioni kwa mwezi na atakuwa ndiye kocha anayelipwa vizuri kuliko wengine wote Ligi Kuu Bara.

Kocha huyo aliyetambulishwa juzi mbele ya wanahabari kabla ya kusainishwa mkataba akiwa na msaidizi wake, ambaye ni mwalimu wa viungo, Mohammed Habib Aymen kutoka Tunisia, inaelezwa atakuwa anavuta mkwanja wa nguvu.


Ingawa mabosi wa Simba wamekuwa wasiri kuanika kiwango cha mshahara kwa madai ni masuala ya siri ya mkataba wao, lakini Mfaransa huyo kawafunika Mzambia wa Yanga na Mromani wa Azam, Aristica Cioaba na wa Singida United, Hans Pluijm.

Lechantre anayechukua nafasi ya Joseph Omog aliyetimuliwa Simba mwishoni mwa mwaka jana, anachosubiri kwa sasa ni kukamilishiwa vibali vya kufanyia kazi na cha kuishi hapa nchini na mara moja atajiunga na timu hiyo.

Inadaiwa Lwandamina anavuta kiasi kisichopungua Sh18 milioni kwa mwezi ikiwa ni kiwango cha Dola 8,000 anazolipwa, huku Cioaba ikielezwa anavuta Sh20 milioni, huku Pluijm akitajwa kama ndiye aliyekuwa kinara analipwa mkwanja mnene, japo inafanywa siri kubwa na mabosi wa timu hiyo iliyorejea VPL msimu huu.


Lakini, wote hao kwa sasa inabidi watulie tu kwa Lechantre kwani, ndiye atakayekuwa akivuta mkwanja mnene kutokana na mkataba alioingia na Simba chini ya tajiri wao, Mohammed ‘Mo’ Dewji.
Mmoja wa viongozi wa Simba aliyeshughulikia dili zima la Lechantre alisema, si vyema kuzungumzia mkataba wa mtu kwani ni makubaliano ya muajiri na muajiriwa, lakini ninachojua kuwa analipwa pesa nyingi zaidi ya makocha wote.


“Si vizuri kutaja pesa hiyo ila tunamlipa zaidi ya hao na pesa yake haipungui chini ya Sh30 milioni kwa mwezi kwani, ni kocha mkubwa kwa hapa Afrika tofauti na hao,” alisema kigogo huyo wa Simba, ikiwa na maana kwa dakika moja atakuwa anavuta si chini ya Sh42,000 kwani kwa siku atavuta zaidi ya Sh1 milioni.
Kiwango hicho kwa dakika moja ni sawa na kuvuta Sh42,000 kinaweza kumrahisishia maisha kwa mtu wa kima cha chini akatumia fedha hizo hata kwa wiki kujikimu kama hana familia au hata mwenye familia.


Mjumbe wa Kamati ya Mabadiliko wa Simba, Mulamu Nghambi aliyekuwa pia miongoni mwa walioshughulikia ujio wa Mfaransa huyo, alisema Lenchatre ni kocha wa kiwango cha juu hapa nchini hivyo hata malipo yake yatakuwa juu.
Alisema walimchukua kocha huyo kutoka kampuni ya (One Match Pro) ya Ubeligiji inayowamiliki makocha wakubwa Afrika kama Herve Renard, ambaye ana historia kubwa ya soka la Afrika pamoja wengine wakali.


“Tulizungumza na kampuni hiyo ndio tulikubaliana kila kitu juu ya mkataba na malipo ya Lechantre, aliyekuja nchini akiwa na msaidizi wake na wakala wa kampuni aliyemtaja kwa kuwa ni Joseph Tenga, aliyesimamia kusaini kwa mkataba huo,” alisema na kuongeza:
“CV ya kocha ni kubwa kwa hiyo hata malipo yake yatakuwa makubwa kuliko ya kocha wowote aliokuwepo hapa nchini na haitakuwa sawa kimalipo na makocha wengine.”
Imetoka Mwanaspoti Jumapili
Share To:

msumbanews

Post A Comment: