Hali  mbaya ya mafuriko yanayoendela kuathiri wananchi wa Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro yamemfanya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Generali Venance Mabeyo kufika Kilosa na kutembelea baadhi ya maeneo yaliyoathirika ili kutafuta ufumbuzi wa pamoja wa kuokoa maisha ya wananchi wa maeneo hayo na mali zao.

Generali Mabeyo aliwasili Kilosa Jan.19, 2018 majira ya jioni na kuungana na mwenyeji wake Dkt. Kebwe Stephen Kebwe Mkuu wa Mkoa wa Morogoro aliyepiga kambi Wilayani humo kwa ajili ya mafuriko hayo kisha bila kujali mvua iliyokuwa inaendelea kunyesha muda wote wakatembelea baadhi ya  maeneo yaliyoakuwa yamethiriwa ili kuona hali halisi ya mafuriko hayo.

Kwenye kikao cha majumuisho Mkuu huyo wa Majeshi nchini alishauri kuwa ili kutatua changamoto hiyo inatakiwa nguvu ya ziada na ya pamoja kwa taasisi zote kuungana, Ikiwa ni pamoja na taasisi mbali ili kuweza kuokoa maisha ya watu, mali zao pamoja na miundombinu iliyoathiriwa.

Hata hivyo alisema changamoto hiyo inatakiwa kuwe na mpango wa muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu. Amesema suluhisho la mpango wa mda mfupi ni kuwa na kazi ya dharura, na kazi hiyo ya dharura inahitajika kuwepo na mpango wa dharura ambao ni kuokoa maisha ya watu waliozingirwa na maji ili wasiendelee kukosa huduma za kijamii na pia kuathiri afya zao kwa kunywa maji ambayo si salama.

Pamoja na kuwepo kwa wazo la kurekebisha tuta la mto Mkondoa ikiwa ni mpango wa muda wa kati ili maji hayo yafuate mkondo wake lakini pia Generali Mabeyo ameshauri kuangalia namna ya kupunguza kasi ya maji hayo kuanzia yanakotoka kwa kujenga mabwawa ikiwa ni mpango wa muda mrefu.

“Maji haya yanakuja huku ni kama sisi ni waathirika zaidi lakini yanakoanzia hatujui hali iko namna gani, pengine katika mpango wa muda mrefu ingetazamwa namna ya kuyapunguza haya maji kasi yake.Sasa katika kuyapunguza, taasisi mablimbali zina wataalamu ambao wanaweza kusaidia kuweza kujenga mabwawa makubwa huko yanakoanzia ili haya maji  kupunguza kasi yake kabla hayajafika huku” alisema Generali Mabeyo.

Akitoa maelezo ya awali Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Stephen Kebwe amesema tuta hilo la mto Mkondoa lilijengwa enzi za Mkoloni kama kinga kwa  mji wa Kilosa na kwa mara ya kwanza lilipasuka mwaka 2010. Ujenzi  wake kuanzia hapo haukukamilika vizuri kutokan na hali ya kifedha na sasa limepasuka baada ya Mvua nyingi kunyesha kuamkia Jan,11 mwaka huu.

Hata hivyo Dkt. Kebwe ametoa Ombi kwa Mkuu huyo wa Majeshi, kupata nguvu kazi ya wananjeshi, vifaa na utaalamu wao ili baada ya mvua hizi kupungua waendelee na kutafuta mbinu ya kuuongoza mto Mkondoa uweze kupita katika sehemu yake ya awali na hivyo kutoathiri wananchi, mali zao na miundombinu iliyopo eneo hilo .

Share To:

msumbanews

Post A Comment: