Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Zanzibar, Salum Mwalimu amefanikiwa kurudisha fomu ya kugombea Ubunge jimbo la Kinondoni huku akiwataka wanachama wa chama hicho kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha muda mfupi.
Mhe. Salum ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari vilivyoweza kujitokeza katika ofisi za Tume ya Uchaguzi Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam leo alasiri(Jumamosi).
"Nimefarijika kwamba fomu imepokelewa na haina mapungufu yeyote yale, kwa hiyo hatuna shaka lolote katika fomu yetu kwa maana tumeikagua na kuuliza maswali katika kipengele jinsi tulivyojaza na wakatujibu tupo sahihi. Imani yangu ni kwamba hawajaona kosa ambalo wanaweza kulikalia kimya walisubiri ili lilete matatizo baadae", alisema Mhe. Salum Mwalimu.
Aidha, Mhe. Salum aliendelea kufafanua baadhi ya mambo kwa kusema hatoweza kutangaza siku ya kuanza kampeni rasmi mpaka itakapofika alasiri ya kesho (Jumapili) kwa maana muda huu wa katikati ameuacha ili kama kutakuwa na watu waweze kuweka mapingamizi yao.
"Kwa hiyo baada ya muda huo kupita siku ya kesho bila ya shaka nitakuwa mgombea rasmi wa jimbo la Kinondoni ambaye nisiyekuwa na doa kwa ajili ya mapambano hayo", alisistiza Mhe. Salum Mwalimu.
Pamoja na hayo, Mhe. Salum aliendelea kwa kusema "kikubwa labda niwaambie hatukuja ku-beep wala hatu-beep kamwe haitakuja kutokea ku-beep katika jimbo la Kinondoni. Tunamaanisha na tunaamini kabisa kama nidhamu ya siasa waliyoikataa, hapa watairudisha na wasipoikubali kuirudisha Kinondoni maana yake ustaarabu katika siasa tunaamini utakuwa umekwishamalizika. Hatutokuwa wa kulia, safarii hii ikibidi tutawasababisha wale waliosababisha sisi tunalialia wao ndio walie".
Kwa upande mwingine Mhe. Salum Mwalimu amesema amedhamilia na amejitoa kusimamia haki ya wananchi wa Jimbo la Kinondoni na kuahidi hatoweza kuyumba katika hilo
Post A Comment: