Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema ameshangazwa na kauli ya Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Elizabeth Mkwizu kwamba hakuna rufaa ya uchaguzi wa Jimbo la Longido mahakamani hapo.
Elizabeth akizungumza na Mwananchi juzi alisema, “Hapa hatuna rufaa ya uchaguzi wa Jimbo la Longido, bali kuna maombi ya kuongezwa muda wa kuwasilisha ‘notice of appeal’ (taarifa ya kusudio la kukata rufaa). Walileta notice of appeal lakini ikatupiliwa mbali, sasa wanaomba muda ili waiwasilishe tena. Maombi si rufaa, kwa hiyo haya maombi yasingeweza kusimamisha shughuli za uchaguzi.”
Hata hivyo, Mbowe akizungumza na mwandishi wetu jana alisema kuna vitu vinaendelea kwa namna moja au nyingine katika Mahakama vinafikirisha na kuona wapinzani hawatendewi haki.
“Kama wanakiri maombi yalipelekwa na wanayo, kufungua kesi si ni ‘process’ (mchakato), zote za kwenda kukata rufaa sasa kama maombi yatakubaliwa na tukakata rufaa, huo uchaguzi ulioitishwa na kufanyika inakuwaje?” alihoji;
“Hakuna mtu anayetaka kukata rufaa bila sababu, maombi hayo ni sehemu ya kesi. Lakini kwa nini wasingesikiliza haraka hayo maombi ili kama yanakataliwa uchaguzi ufanyike.”
Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alisema, “Kuna mambo ambayo yafanyika katika Mahakama zetu baadhi yanatia doa na ndilo tatizo la nchi yetu.”
Katika ufafanuzi wake, Mkwizu alisema kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Mahakama ya Rufaa, maombi hayo yamepangwa kusikilizwa na Jaji Jacob Mwambegele, Februari 5.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: