kocha Mecky Maxime

kocha Mecky Maxime 
Dar es Salaam. Licha ya Kagera Sugar kupata matokeo mabaya katika Ligi Kuu Tanzania Bara, kocha Mecky Maxime amesema hakuna hujuma katika mechi za timu hiyo na ameahidi kupambana hadi dakika ya mwisho.
Akizungumza kwa simu jana, Maxime alisema ataendelea kuipigania Kagera Sugar katika mechi za mzunguko wa pili kwa kuwa ana kikosi ‘imara’.
Alisema matokeo inayopata timu hiyo ni changamoto kwake, lakini hana mpango wa kukata tamaa katika kampeni ya kuinusuru na janga la kucheza mchangani msimu ujao.
Nahodha huyo wa zamani wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’, alisema ana amini mzunguko wa pili utakuwa na manufaa kwake, baada ya kufanya marekebisho ya kasoro zilizojitokeza awali.
Maxime ametoa kauli hiyo baada ya Kagera Sugar juzi kulala bao 1-0 ugenini dhidi ya Njombe Mji kwenye Uwanja wa Sabasaba na kujiweka katika mazingira magumu kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Kagera Sugar imeshinda michezo miwili kati ya 13 iliyocheza hadi sasa huku ikiwa imetoka sare mara sita na kufungwa mechi tano.
“Mpira ndivyo ulivyo, lakini bado hatujakatishwa tamaa na matokeo hayo. Hatuna tatizo kuna watu wanaweza kudhani kuna kitu nyuma ya pazia kinachosababisha matokeo hayo, lakini hakuna na tunafungwa kwa kuzidiwa mpira tu,” alisema Maxime.
Kocha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar alisema hakuna njama dhidi ya Kagera Sugar kwa kuwa mpira una matokeo matatu, hivyo anajipanga kwa mechi zinazofuata.
“Tunahitaji kupata matokeo mazuri na kila mtu anaumizwa na kinachoendelea kwenye timu yetu, lakini tunajipanga na ninaamini mzunguko wa pili mambo yatakuwa sawa,” alisisitiza Maxime.
Timu ya Simba inaongoza Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 26 sawa na Azam lakini ina uwiano mzuri wa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: