WAGENI watakaohudhuria "sherehe" za msiba wa mama mzazi wa Askofu Mkuu  wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, aliyefariki dunia Jumapili iliyopita wamewekewa masharti ya kuvaa kinadhifu msibani hapo.Aidha, Askofu Gwajima alitangaza hangesita kumfukuza kwenye shughuli hiyo mgeni yeyote ambaye angefika akiwa amevaa fulana ziliozoandikwa "mambo ya ajabu ajabu".
Mama mzazi wa Askofu Gwajima, Ruth Basondole (84), aliagwa juzi nyumbani kwa askofu huyo jijini Dar es Salaam na sherehe hizo zitafanyika leo Tegeta Salasala.
Katika ujumbe wa sauti uliosambaa kwenye mitandao ya kijamii juzi, Askofu Gwajima aliwataka wale watakaohudhuria sherehe hizo zinazofanyika nyumbani kwake Tegeta wavae mavazi nadhifu.
Pia alipiga marufuku mtu kufika huko akiwa amevaa fulana zilizoandikwa Pumzika Kwa Amani au zenye ujumbe wa Tutakukumbuka.

Badala yake, Askofu Gwajima ameruhusu wageni watakaopenda kuvaa vazi hilo, kufika na fulana zenye maandishi kama Shujaa Hongera au Shujaa Umerudi Nyumbani.
"Kwa hakika kabisa ni wakati wa sherehe," alisema Askofu Gwajima katika ujumbe huo na kwamba "ni 'ku-celebrate (kufurahia), ni kucheza, ni kuimba, ni kuvaa vizuri... funga tai.
"Hatutaki namna ya kuvaa masempelesempele hiyo mtu amevaa, amejifunika funika... tuvae kwa namna nzuri (maana) ni sherehe kama zilivyo sherehe nyingine kabisa.
"Halafu naomba niwajulishe kuepusha matisheti (fulana), mtu atakayekuja na matisheti yaliyoandikwa vitu vya ajabu ajabu namtimulia mbali.
"Sitaki matisheti ya Rest In Peace (Pumzika Kwa Amani), matisheti ya sijui Tutakukumbuka hapana."

Alisema anataka tisheti ziwe na ujumbe unaoonyesha mtu amekwenda mbinguni.
Alitaka katika msiba huo watu wacheze, waimbe na uwe muda mzuri wa kujengana kiroho pia.
Askofu huyo alisema mama yake amekwenda mbinguni tukio ambalo linamfanya awe na amani ya kweli.

"Mama alikuwa anajua anakwenda mbinguni kama miezi miwili au mitatu hivi (iliyopita), hivyo hizi ni sherehe kwa hakika kabisa," alisema.
"Hili ni tukio la furaha, tucheze, tuimbe mimi mwenyewe nina furaha..."
Kwa utamaduni wa Mtanzania huwa hakuna masharti ya mavazi katika misiba, isipokuwa sare kwa ndugu wa karibu na marafiki wa marehemu.

Aidha, kutokana na utamaduni huo ambapo msiba huchukuliwa kama tukio la huzuni, waombolezaji huweka nyuma unadhifu ambapo wengi huvaa tisheti zilizoandikwa ujumbe wa huzuni na nguo za 'masempelesempele'.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: