Wananchi wa Kata ya Itewe, Chunya mkoani Mbeya, wameanza mkakati maalumu wa kuanzisha kiwanda cha kusindika mapapai ifikapo mwaka 2020 kwa kuanza uzalishaji wa zao hilo, ili kuwa na uhakika wa malighafi.

Katika kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa, Diwani wa Kata hiyo, Alex Kinyamagoha, ambaye ndiye mhamasishaji mkuu wa kilimo cha zao hilo, amegawa zaidi ya miche 10,000 kwa wananchi, ili waanze kupanda kwenye mashamba yao na kwenye makazi.

Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa kugawa miche hiyo, akiwa ameambatana na baadhi ya wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Tawi la Mbeya, Kinyamagoha alisema kiwanda hicho kitakuwa sehemu ya wananchi hao kuunga mkono kauli ya Rais Dk. John Magufuli kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Alisema kila mwananchi ameelimishwa na kuhamasishwa kuzalisha matunda hayo kwa maelezo kuwa zao hilo licha ya kusaidia malighafi kwa ajili ya kiwanda, pia litasaidia kuongeza kipato.
Alisema lengo la mradi huo kwa sasa ni kuanza na kila kaya kupanda miche mitano na baada ya hapo kuanzisha mashamba makubwa, ili kuongeza tija.

“Uchumi wa viwanda hutegemea mapinduzi ya kilimo. Mazao yatokanayo na kilimo ndiyo malighafi zinazotumika katika viwanda, hivyo lazima tuonyeshe mfano kwa kuzalisha matunda haya ili tutimize lengo la kuanzisha kiwanda,” alisema.

Alisema iwapo mipango yao itafanikiwa, wanataka kuhamasisha kata zingine za Wilaya ya Chunya kuzalisha matunda hayo, ili miaka ijayo wilaya itambulike kwa zao hilo kama ilivyo kwa Wilaya ya Rungwee inayotambulika kwa kuzalisha ndizi kwa wingi.

Mmoja wa wasomi kutoka katika Chuo Kikuu cha Mzumbe waliohudhuria hafla ya kugawa miche hiyo, Aidan Ndunguru, aliwataka wananchi hao kuipanda na kuitunza vizuri ili kufikia lengo.

Alisema baada ya miaka kadhaa, kata hiyo itakuwa ya mfano endapo watatunza vizuri miche hiyo na kwamba manufaa watakayoyapata yatakuwa makubwa kuliko mazao mengine wanayozalisha.
Ndunguru alisema wageni watakaokuwa wanaingia katika wilaya hiyo watakuwa wananunua matunda hayo na kwenda kuitangaza wilaya wanakokwenda.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: