SHAHIDI wa nne wa Jamhuri, askari polisi mweye namba H 2261, Monga (25), ameiambia Mahakama ya Wilaya ya Arusha kuwa aliposikia Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), akitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Rais katika mkutano wa hadhara eneo la Kambi ya Fisi, alipata hisia za machafuko.

Akitoa ushahidi huo mbele ya Hakimu Devotha Msofe, alisema alifika katika mkutano wa hadhara Oktoba 22, mwaka 2016 eneo la Kambi ya Fisi baada ya kutumwa na mkuu wake wa upelelezi akamsikilize mbunge huyo. 

“Nilipofika pale nikiwa na video kamera nilimsikia Lema akisema: “Mheshimiwa Rais akiendelea kudhalilisha demokrasia na vyama vya upinzani basi ipo siku nchi itaingia kwenye umwagaji wa damu na wananchi watajazwa vifua na siku vitapasuka.”

Alidai Lema aliendelea kusema polisi na majeshi hawataweza kuzuia uhalifu utakaojitokeza na nchi imeandaliwa kuingia katika udikteta wa mwanaume mmoja, hivyo hatutaweza valishwa sketi tukiwa ndani ya suruali.

 Alidai kutokana na maneno hayo, Lema alifanya wananchi kuwa na shaka na kauli hiyo. Mahojiano kati ya wakili wa upande wa utetezi na shahidi huyo yalikuwa kama ifuatavyo: 


Wakili: Baada ya kurekodi una hakika hivyo video bado vipo? 

Shahidi: Sina hakika kama ipo, ila nina imani vitakuwapo sababu vifaa vyote vimekabidhiwa kwa ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, Damas 

Massawe. Wakili: Ulipata hisia gani baada ya kusikia hayo maneno?

 Shahidi: Nilipata hisia ya kupelekea machafuko. 

Wakili: Kuna maelezo kuwa kuna mtu kaoteshwa  Rais atakufa, je, kauli hiyo inasababisha ilete vurugu? 

Shahidi: Sikusikia na sikuwapo.

Wakili: Je, clip ya video uliipitia ulipotoka mkutanoni? 

Shahidi: Hapana. Baada ya mahojiano hayo alisimama shahidi wa tano ambaye ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi na Mkaguzi wa Oparesheni za Polisi Jiji la Arusha, Joseph Lubia (33) na kuieleza mahakama kuwa maneno ya Lema yalimpa hisia mbaya na kupelekea kusababisha watu kuvunja sheria. Alipoulizwa na wakili upande wa utetezi, John Mallya, kama kuna mtu anakatazwa kuota ndoto, alidai hakuna anayekatazwa. Baada ya mahojiano hayo hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi leo itakapoendelea kusikiliza ushahidi mwingine.

Kesi hiyo 440 ya mwaka 2916 inayomkabili Lema, anayedaiwa kutoa maneno ya uchochezi na udhalilishaji kwa Rais John Magufuli, eneo la Kambi ya Fisi ambapo inadaiwa alitamka Rais Magufuli asipoacha kiburi chake cha kuminya demokrasia atakufa kabla ya mwaka 2020. 
Share To:

msumbanews

Post A Comment: