WAKATI kampeni za uchaguzi mdogo wa marudio ya ubunge Jimbo la Siha zikiwa zimeanza kushika kasi,  vijana 1,483 wamekubali kukihama chama cha zamani cha Dk. Godwin Mollel, Chadema, na kuunga mkono harakati zake za kurudi Dodoma kupitia Chama cha Mapinduzi.


Mollel alitangaza ujio wa vijana juzi, akidai wanatoka Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) Wilaya ya Siha.
Mgombea huyo wa CCM sasa alikuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Lawate, kata ya Kirua.

“Makamanda waliokuwa wakiniunga mkono nikiwa chama kile cha zamani (Chadema) kabla sijajiuzulu wanakuja kuniunga mkono, wapo 1,483," alisema Dk. Mollel ambaye alijiuzulu ubunge mwishoni mwa mwaka jana ili kumuunga mkono Rais John Magufuli.

"Sitawachukia ambao hawataniunga mkono kwa sababu wote ni wananchi wangu kama nikichaguliwa.”Kabla ya Dk. Mollel kudai amekamilisha mipango hiyo ya kuvuna vijana wa upinzani, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Rodrick Mpogolo alisema licha ya Chadema na vyama vya CUF na Chausta kusimamisha wagombea katika uchaguzi huo, hakuna ubishi mgombea wao atashinda kwa kishindo.

"CCM haiongozi nchi kwa kubahatisha... inakubalika kwa sababu ina ajenda zinazotekelezeka na kama wananchi mnahitaji maendeleo, chagueni wagombea wa CCM," alisema Mpogolo. "Lakini kama mnahitaji maigizo wanaSiha mchagueni mbunge anayetoka upinzani."
Naibu katibu mkuu huyo alisema CCM itaendelea kuleta maendeleo kwa wananchi wa Siha kwa haraka na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja endapo watamchagua Dk. Godwin Mollel.
Kwa upande wake, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole alisema Chadema siyo chama kinachoweza kuwaletea wananchi maendeleo.

Alisema chama hicho kimekuwa kikifanya mchezo na akili za Watanzania kwa kujinufaisha matumbo yao na familia zao na kuwataka kutofanya makosa ya kumchagua mgombea wa chama hicho.
Polepole alisema Chadema ni chama cha wapigadili na ndiyo maana wabunge wa chama hicho wamezuiwa kuzungumza na viongozi wa CCM ambao ndiyo serikali na kusababisha maendeleo ya wananchi kurudi nyuma.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: