Serikali imesema kuwa ilitoa jina la Ndugai kwa faru mmoja (Faru Ndugai) katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kunatokana na kiongozi huyo wa bunge kuwa mhifadhi, pia alikuwa mjumbe wa bodi ya Ngorongoro kwa muda mrefu.
Hayo yalisemwa jana na Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dkt Fredy Manongi alipokuwa akiongea na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii waliotembelea hifadhi hiyo.
Kiongozi huyo alilamizika kuyasema hayo baada ya Mbunge  wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (CHADEMA) na Mbunge wa Geita Mjini, Joseph Msukuma (CCM)  waliotaka kujua mchakato unaotumika kuwapa wanyamapori majina ya viongozi au watu maarufu.
Wabunge hao walihoji hilo baada ya kuwapo kwa baadhi ya wanyama wenye majina ya viongozi akiwemo Faru Ndugai, aliyebeba jina la Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai.
Aidha, katika hatua nyingine, Dkt Manongi amesema kuwa, mamlaka hiyo inaandaa utaratibu wa kisheria utakaowawezesha watu mashuhuri kulipia kiasi cha fedha ambacho hakukitaja endapo watataka wanyama katika hifadhi hiyo kupewa majina yao.
Hatua hiyo imepongezwa na watu mbalimbali wakisema kuwa, kwa kufanya hivyo mamlaka hiyo itaweza kuongeza mapato yake lakini pia kuboresha huduma za utalii.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: