Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wametoa onyo kwa madereva wa daladala watakaoendelea kukatisha ruti katika jiji la Dar es salaam.

Kauli hiyo imetolewa leo Januari 17,2018 jijini Dar es Salaam, kupitia ziara ya uelimishaji wa madereva wa daladala katika matumizi ya njia mpya zinazotarajiwa kufunguliwa Januari 29 mwaka huu ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na changamoto ya usafiri.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Salomon Mwangamilo amesema msako na adhabu kali zitaendelea kuchukuliwa ikiwa ni sehemu ya kukomesha tabia za madereva wasiofuata utaratibu.

"Atakayechagua ruti namba moja au namba mbili apite kwa kuzingatia maelekezo ya Sumatra, sasa hivi tutaongeza adhabu na tutaanza na wale watakaotaka kutujaribu, utaratibu uzingatiwe ili kuepukana na kero kwa abiria," amesema Kamanda Mwangamilo.

Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri barabarani kutoka Sumatra, Johanes Kahatano amesema sababu nyingine ya kufungua njia mpya ni kukabiliana na kero ya ukatishaji wa njia hatua inayoibua kero kwa abiria.

"Njia hizo zitaboresha huduma kwa kuongeza huduma katika njia mpya, mji unapanuka na kuondoa kero ya ukatishaji wa njia, utozaji wa nauli zisizoruhusiwa kisheria, kupunguza msongamano wa vituo vya daladala," amesema Kahatano.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: