Mashahidi watatu kati ya saba wa upande wa mashtaka wametoa ushahidi wao dhidi ya mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu na katibu wa Chadema wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga.

Sugu na Masonga wanashtakiwa kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli, wakidaiwa kutoa maneno hayo Desemba 30 mwaka jana katika mkutano wao wa hadhara walioufanya kwenye viwanja vya Shule ya Msingi ya Mwenge.

Awali, Wakili wa Serikali, Joseph Pande aliiambia mahakama hiyo kwamba wanakusudia kupeleka mashahidi wasiopungua saba pamoja na vielelezo vitano, huku zikiwasilishwa nyaraka za barua zilizotumika kuombea mkutano pamoja na barua za kuwaruhusu kufanya mkutano huo.

Mkuu wa polisi wa Wilaya ya Mbeya, James Chacha alikuwa shahidi wa kwanza kutoa ushahidi wake jana na aliongozwa na mawakili wa Jamhuri, Joseph Pande, Baraka Mgaya na Ofmed Mtenga.

Katika ushahidi wake, Chacha aliieleza mahakama hiyo kwamba yeye ndiye aliyetoa barua ya viongozi hao kufanya mkutano wao wa hadhara baada ya kutimiza masharti na kuridhika na maudhui waliyoainisha katika barua ya maombi hayo.

Alisema miongoni mwa ajenda walizokusudia kuzungumza katika mkutano huo ni Mbunge Sugu kuwaeleza shughuli za maendeleo alizozifanya katika utumishi wake wa ubunge pamoja na kutoa salamu za mwaka mpya.

“Katiba barua yangu ya kuwaruhusu kufanya mkutano ule, niliwaelekeza kwa maandishi mambo wanayopaswa kuyazingatia ikiwa ni pamoja kutotumia lugha ya matusi, kufedhehesha au ya viashiria vyovyote vile vinavyoweza kuvunja amani na usalama wa nchi,” alidai shahidi huyo.

Shahidi wa pili, ambaye ni mkazi wa Soweto jijini Mbeya, Boniface Mwaitorola alidai mahakamani hapo, siku ya tukio alikuwa jirani na viwanja vya shule hiyo na ilipofika saa 10:00 jioni alisogea eneo hilo kwa lengo la kumsikiliza mbunge wake.

Alidai katika mkutano huo awali kabla ya Sugu na Masonga kuwasili eneo la hilo kulikuwa na shamrashamra za watu na muda mfupi viongozi hao waliwasili na Masonga ndiye aliyemkaribisha Sugu kuhutubia lakini kabla yake, kuna maneno aliyotamka Masonga ambayo yalisababisha watu kugawanyika makundi mawili.

Shahidi wa tatu, askari polisi anayefanya kazi ofisi ya upelelezi mkoa wa Mbeya, William Nyamakomage aliieleza mahakama hiyo kwamba siku ya tukio alikuwa nyumbani kwamba na muda mfupi alipigiwa simu na mkuu wake wa kazi (Mkuu wa upelelezi mkoa wa Mbeya) akimtaarifu kuhusu kuwepo kwa mbunge huyo kufanya mkutano wa hadhara hivyo anahitaji kufika eneo hilo kwa ajili ya shughuli kuangalia usalama na kukusanya ushahidi wa lolote litakalotokea kama ni la uvunjifu wa amani jambo alililofanya.

Baada ya shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Michael Mteite aliiahirisha kesi hadi leo itapoendelea na upande wa Jamhuri kuwasilisha ushahidi wao na Sugu na Masonga kurudishwa mahabusu.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: