Watu wengi wamekuwa wakisoma kwa malengo maalum. Japo wengi huchagua kusomea taaluma fulani kwa kuwa ina soko kubwa la ajira na kuwa na malipo mazuri ya mishahara.

Hakuna anayependa kusomea taaluma ambayo anajua wazi kuwa haitomnufaisha katika maisha yake. hivyo wengi wamekuwa makini sana katika uchaguzi wa taaluma ya kusomea.
Zipo taaluma mbalimbali ambazo huwa zinahitajika sana katika sekta tofauti tofauti na huwa na mishahara mikubwa.
Ripoti ya utafiti wa ajira na kipato ya mwaka 2015 (EES 2015) iliyochapishwa mtandaoni hivi karibuni na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) inabainisha kuwa sekta ya huduma za kibenki na bima ndiyo inayolipa zaidi nchini baada ya kundi kubwa la wafanyakazi wake kulipwa mshahara wa zaidi ya Tsh1.5 milioni kwa mwezi. Utafiti huo unaeleza kuwa kwa kila wafanyakazi watatu wa huduma za benki na bima mmoja anapata mshahara huo, kiwango ambacho ni kikubwa mara tano ya kima cha chini cha mshahara kilichowekwa na Serikali cha Tsh310, 000.
Benki na bima inafuatiwa kwa mbali na sekta ya madini ambayo asilimia 5.9 ya wanyakazi wake wanapata mshahara wa kiwango hicho ikiwa na maana kuwa watu sita kwa kila 100 wanauhakika wa kupata zaidi ya Tsh1.5 milioni kwa mwezi. Sekta nyingine zinazofuatia kwa kiwango hicho cha mshahara ni shughuli za utawala wa umma, ulinzi na hifadhi za jamii kwa asilimia 5.2 na afya na ustawi wa jamii kwa asilimia 4.4.
Sekta nyingine zinazolipa vizuri ni pamoja na sekta ya elimu, Afya, huduma za kijamii pamoja na usafirishaji na ujenzi.
Wafanyakazi 8 kati ya kumi katika sekta ya elimu, wanalipwa mshahra wa kati ya Tsh. 300,000 mpaka Tsh. 900,000 sawa na asilimia 75 ya wafanyakazi wote katika sekta hiyo.
Uchambuzi zaidi wa takwimu hizo unaonyesha hata kama sekta ya benki na bima itapimwa kwa mshahara zaidi ya Tsh900, 000 kwa mwezi bado inazidi zote kwani nusu ya wafanyakazi wanapata kiwango hicho.
Hata wakati kukiwa na sekta zinazoonekana kulipa zaidi, ripoti hiyo inaonyesha kuwa sekta ya huduma za malazi na chakula inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanaolipwa mshahara mdogo usiozidi Sh100, 000 kwa mwezi ambao ni sawa na asilimia 29.4.
Utafiti huo, uliofanywa kati ya Julai na Desemba 2015, unaonyesha wafanyakazi 6 kati ya 10 wa sekta hiyo wanalipwa mshahara usiozidi Tsh150, 000 wakifuatiwa na huduma za usaidizi ofisini na sekta ya kilimo, misitu na uvuvi.
Wataalamu wa masuala ya rasilimali watu wanasema kiwango cha mishahara katika sekta husika huwekwa kwa kuangalia vigezo mbalimbali vikiwemo aina ya elimu na ujuzi unaohitajika.
Mtaalamu nguli wa masuala ya rasilimali watu, Zuhura Muro alieleza kuwa kiwango na tija katika uzalishaji, kiwango cha ujuzi na elimu na ushindani uliopo katika sekta husika huchangia kwa kiasi kikubwa kubaini viwango vya mishahara.
“Mtu mwenye elimu ya chini katika sekta ya benki na bima ni ngazi ya cheti kwa kuwa ina vihatarishi vingi na inadhibitiwa sana ndani na kimataifa. Huwezi kuajiri mtu yeyote tu katika sekta hiyo ndiyo maana mishahara ni mikubwa,” alisema Muro ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya masuala ya rasilimali watu ya Kazi Services Limited.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: