Alikiba ni miongoni mwa wasanii wakubwa nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Hapa nyumbani Tanzania, amekuwa akishindanishwa sana na Diamond Platnumz. Pia, amejitahidi na kuweza kutoshuka katika muziki tangu alipoanza kuliteka soko la Tanzania na kujulikana kama msanii mkubwa hapa nchini na amewahamasisha vijana wengi sana kuingia katika tasnia hiyo.
Jina lake rasmi ni Ali Saleh Kiba, lakini anafahamika zaidi kwa jina la sanaa la Alikiba au King Kiba. Alizaliwa Novemba 26 mwaka 1986 mkoani Iringa, Tanzania. Ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wanne wa Mzee Saleh Omary na Tombwe Njere. Ndugu zake wengine ni Abdulkiba, Zabibu Kiba na Abuu Kiba.
Alikiba ni mwandishi wa mashairi bali pia ni mwimbaji. Kazi zake zimekuwa zikisimamiwa na Rockstar4000 lakini pia Mei 20 mwaka 2016 alisaini mkataba na kampuni ya Sony Music Entertainment ya nchini Marekani kwa ajili ya kusimamia kazi zake.
Akiwa anasoma Shule ya Msingi Upanga, alipenda sana kuimba katika matamasha ya vipaji na sherehe mbalimbali shuleni hapo. Baada ya kumaliza Elimu ya A-level mwaka 2004 aliamua kuweka nguvu zake katika muziki na kutoa ngoma mbalimbali ambapo wimbo wake wa kwanza unaitwa Maria.
Mbali na muziki, Alikiba anacheza mpira wa miguu. Mwaka 2005 alipewa ofa ya kucheza mpira katika timu moja huko Uganda lakini alikataa kwa sababu hilo lilikuwa siyo lengo lake la maisha hivyo aliendelea kukaza buti katika masuala ya muziki.
Mwaka 2007 alitoa albamu ya Cinderella ambayo ilimtambulisha rasmi Tanzania nzima ikiwa na nyimbo mbalimbali ambazo zinapendwa hadi leo kama vile Cinderella.
Alikiba alitoa album yake ya pili iliyokwenda kwa jina la Ali K 4 real mwaka 2008 ambayo ilihitimisha kuweka chapa ya jina lake katika ulimwengu wa muziki Afrika Mashariki na maeneo mengine. Album hiyo ilikuwa na nyimbo nyingi zikiwemo Nakshi Nakshi, Usiniseme.
Mwaka 2010 Alikiba aliendelea kuonyesha kwamba anaujua muziki baada ya kuchaguliwa kushiriki katika ‘project’ ya One 8 ambayo alihusisha wasanii kutoka Afrika pamoja na mwanamuziki R Kelly wa Marekani. Mbali na Alikiba, wasanii wengine wakubwa wa Afrika walioshiriki ni pamoja na Fally Ipupa, 2Face, Amani, Movaizhaleine, 4X4, Navio, JK.
Alikiba amekuwa akishirikiana na wasanii mbalimbali katika kazi za muziki ambapo tayari amefanya kazi na wasanii wa ndani na nje ya Afrika. Miongoni mwa wengi ambao ameshirikiana nao ni pamoja na MI, Profesa Jay, Patoranking, R Kelly, Lady Jaydee, Sauti Soul.
Pia, ametajwa kushiriki lakini ameshinda tuzo mbalimbali barani Afrika na nje. Baadhi ya tuzo alizoshinda ni pamoja na Best Zouk/Rhumba Song (Dushelele), Wimbo Bora wa Mwaka , Video Bora ya Mwaka, Wimbo Bora wa Afro Pop (tuzo zote tatu zikiwa ni kwenye wimbo wa Mwana). Pia ameshinda tuzo ya MTV EMA ya Msanii Bora wa Afrika mwaka 2016, ameshinda tuzo 3 za EATV kupiti wimbo wa Aje mwaka 2016.
Nje na muziki, Alikiba ana watoto watatu lakini bado hajao. Kiba, amewahi kuwa na uhusiano na mjasiriliamali Jokate na Mwegelo na kwa kipindi fulani ilisemekana kuwa kulikuwa na ushawishi kutoka familia ya King Kiba kwamba amuoe mrembo huyo.
Kwa ujumla, Alikiba amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutenganisha maisha yake ya muziki na maisha binafsi. Sio mambo mengi sana yanayofahamika kumhusu yeye katika maisha yake binafsi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: