MKUU wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqqaro, amepiga marufuku waratibu wa elimu kutoka kata za Jiji la Arusha kukaa ofisini na badala yake watembelee shule na kufahamu changamoto wanazokumbana nazo wazazi, wanafunzi na shule kwa ujumla.

Akizungumza jana na walimu wakuu wa shule za msingi, sekondari na waratibu wa elimu kata kwenye kikao cha kukumbushana wajibu wa kazi zao na kuepuka michango isiyostahili kwa wanafunzi, Daqqaro aliwataka wazazi na walezi wenye watoto wanaosoma shule za msingi na sekondari, ambao watozwa fedha za michango iliyopigwa marufuku, kutoa taarifa kwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha ili wachukuliwe hatua.

Alisema baadhi ya waratibu wa elimu kata mbalimbali, wamekuwa na tabia ya kuchukua taarifa za elimu katika taarifa za walimu darasani, badala ya kupita shuleni, kwaajili ya kufanya ukaguzi wa michango isiyostahili mashuleni.

Haiwezekani shule zikatoza michango pasipo kuwashirikisha wazazi au walezi na baadaye kuwafukuza wanafunzi nyumbani pale wanaposhindwa kutoa michango hiyo, huku waratibu wa elimu wakiangalia tu, hii haiwezekani,” alisema.

Alisema suala hilo halikubaliki na aliwaomba wazazi na walezi wa watoto, wawafichue walimu na wanaochangisha michango isiyostahili, kwa kuwa wakati mwingine mtoto anachangishwa fedha za kununua tanki la kuhifadhia maji, wakati hakuna makubaliano hayo na hakuna hatua zinazochukuliwa.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Grayson Orcado, alisema kwa sasa wataanza msako wa nyumba kwa nyumba, ili kubaini wanafunzi wasiofika shuleni, kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha kwanza.

Alisema wanataka kujua sababu zipi zilizowafanya kutohudhuria masomo, ili hali wameandikishwa shule au kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.

Awali mmoja kati ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Olorieni, Eliud Manoya, alisema kabla ya zuio hilo walikuwa wakiwatoza wanafunzi Sh 16,500 kwa ajili ya mchango wa kuchimba shimo la choo, lakini baadaya amri hiyo, watarejesha fedha hizo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: