Uongozi wa Chadema tawi la ukombozi kata ya Saranga wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam,  umemvua uongozi na kumfukuza uanachama katibu wa tawi hilo, Braxson Mwakilanga.

Mwakalinga anadaiwa kujipatia Sh800,000 kutoka kwa wananchi kinyume na taratibu, madai ambayo aliyakanusha na kubainisha kuwa yanatokana na uamuzi wake wa kukihama chama hicho na kujiunga na CCM.

Akizungumza leo Januari 17, 2018 mwenyekiti wa  tawi hilo, Wilkado Mayaruka amesema walikaa kikao cha kamati tendaji Januari 14 mwaka huu kumjadili Mwakilanga, kupendekezwa avuliwe uongozi na uanachama.

Amesema Mwakilanga amekuwa akiwashawishi baadhi ya viongozi wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha) na Baraza la Wanawake (Bawacha) wa tawi hilo kuhamia CCM kwa makubaliano ya kuwapatia kila mmoja Sh1.5milioni.

“Pia amehusika kupokea na kuzitumia fedha za usafiri Sh50,000 kinyume na matumizi ya chama siku ya uchaguzi mdogo wa udiwani Novemba 26 mwaka 2017, hivyo mpaka leo hatujawapatia wahusika,” amesema.

Amesema tuhuma nyingine ni kuwa kikwazo cha migogoro ndani ya tawi hilo bila ya kujali kuwa kufanya hivyo ni kukiumiza chama hicho kikuu cha upinzani  nchini.

Manyaruka amesema licha ya katibu huyo kuitwa kujibu tuhuma zinazomkabili hakufika katika vikao, hakutoa hudhuru yoyote.

Akijibu tuhuma hizo Mwakilanga amesema hajawahi kupewa barua ya kufukuzwa uanachama na tuhuma anazopewa zimeibuka baada ya kusikia amehamia CCM.

Amesema alijiunga CCM Januari 14 mwaka huu baada ya kuridhishwa na utendaji mzuri wa kazi wa Rais John Magufuli.

Kuhusu kuwachangisha wananchi Sh800,000, Mwakalinga alikanusha jambo hilo kwa maelezo kuwa ni siasa za kuchafuana
Share To:

msumbanews

Post A Comment: