Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) inakutana jioni ya leo kujadili mambo kadhaa yanayohusu mwenendo wa Chama hicho na Nchi kwa ujumla.

Kamati hiyo ilikuwa ikutane siku ya jana lakini ikaahirishwa ili kupisha maziko ya Mama Mzazi wa Mkurugenzi wa Sheria wa Chama, Wakili Peter Kibatala aitwaye Anna Mayunga amabyo yalifanyika mkoani Morogoro.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya nje, John Mrema saa kamati hiyo itakutana leo jioni baada ya viongozi wote kurejea kutokea msibani huku akiwa hayupo tayari kuweka bayana ajenda zitakazoongelewa.

Muungwana inafahamu kuwa pamoja na mambo ambayo yatazungumzwa kwenye kikao hicho ni pamoja na suala la aliyekuwa mgombea wao wa Urais katika uchagui mkuu uliopita na mjumbe wa kamati kuu, Edward Lowassa kumtembelea Rais Magufuli ikulu na kumpongeza kwa utendaji kazi wake.

Tangu Lowassa ampongeze Rais kumekuwa na maneno ya lawama na kumshambulia kutoka kwa viongozi, makada na wanachama wa Chadema ambapo Mwenyekiti Mbowe alikaririwa na Radio ya BBC akikana kutambua kauli za Lowassa kama msimamo wa Chama.

Hivyo kikao cha leo kitalenga kujadili kauli hizo za Lowassa lakini pia kwa Mwenyekiti Mbowe kuwapa mrejesho wajumbe wa kamati kuu kile ambacho Lowassa alizungumza ndani na Rais Magufuli hiyo ikiwa ni baada ya Lowassa na Mbowe kukutana na kujadili juu ya tukio hilo.

" Hatuwezi kuzungumza leo kusema Chama kitachukua hatua gani dhidi ya Waziri Mkuu Mstaafu, Lowassa lakini niseme majibu yote ya hatua gani tutachukua yatatolewa baada ya kamati kuu kukutana na Lowassa mwenyewe kutuambia nini hasa alizungumza na Rais Magufuli wakiwa ndani maana tunafahamu yapo mengi yalizungumzwa wakiwa wawili," alisema Salum Mwalimu Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zanzibar.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: