Chama wa Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha kimewataka wakazi wa mjini hapa kuwachagua wagombea wa chama hicho, kwa kuwa CCM ya sasa ni mpya ambayo inalenga kutatua kero za wananchi.


Kudorora kwa chaguzi katika Jimbo la Longido na Kata ya Kimandolu kumetokana na Chadema ambayo ndio ilikuwa inashikilia jimbo na kata hiyo kutosimamisha wagombea ikitaka Tume ya Uchaguzi kuondoa dosari zilizotokana na uchaguzi mdogo uliopita.
Akizungumza katika mikutano ya kampeni katika Kata ya Kimandolu, katibu wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Elias Mpanda aliwaomba wakazi wa Arusha kutambua kuwa chama hicho kwa sasa ni tofauti CCM ya miaka ya nyuma.
“Nakiri chama chetu kilikuwa kinakwenda vibaya, tulitawaliwa na makundi na hivyo kuwapata baadhi ya wagombea wasio na sifa, lakini sasa chini ya mwenyekiti wetu, Rais John Magufuli nadhani mnaona CCM mpya imekuja ambayo imejipanga kutatua kero za wananchi,” alisema.


Alisema CCM imekuwa na ilani bora katika chaguzi zote, lakini kulikuwa na matatizo katika utekelezaji wake jambo ambalo hivi sasa wamelipatia ufumbuzi na ilani yao inatekelezwa.
“Nawaomba mchague wagombea wa CCM ambao wataweza kuisimamia vyema Serikali katika kushughulika na kero za wananchi tofauti na wagombea wa upinzani,” alisema.
Kwa upande wake, katibu wa siasa na uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaaban Mdoe alisema ilani ambayo inatekelezwa nchini ni ya chama chao.
“Msidanganywe na wapinzani, hawana jipya chagueni CCM kwa maendeleo yenu,” alisema Mdoe


Aliyekuwa diwani wa Chadema katika kata hiyo, mchungaji Rayson Ngowi alisema aliamua kujiuzuru udiwani na kujiondoa katika chama hicho kisha akajiunga CCM baada ya kuona siasa za upinzani hazina tija tena.
“Ndugu zangu mliobaki Chadema ondokeni, siasa za upinzani hazina tija tena, Serikali ya Rais John Magufuli inatatua kero zote ambazo tumekuwa tukilalamika lakini pia hakuna uwazi katika upinzani,” alisema.


Katika uchaguzi ambao unatarajiwa kufanyika Januari 13, CCM imemrejesha aliyekuwa mgombea wake wa ubunge katika uchaguzi wa 2015, Dk Stevin Kiluswa kugombea Longido baada ya aliyekuwa mbunge, Onesmo Ole Nangole (Chadema) kuvuliwa ubunge na mahakama.
Katika Kata ya Kimandulu, baada ya kujiuzuru mchungaji Ngowi CCM imempitisha Gaudence Lyimo ambaye aliwahi kwa meya wa Jiji la Arusha kugombea udiwani.

Chanzo: Mwananchi
Share To:

msumbanews

Post A Comment: