Hafla ya kusainiana mkataba imefanyika leo Makao Makuu ya NMB yaliyopo Posta, jijini Dar es Salaam, ambapo Azam FC iliwakilishwa na mmoja ya Wakurugenzi wa timu hiyo, Yusuf Bakhresa, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Azam Media Ltd, na Ofisa Mtendaji Mkuu, Abdul Mohamed huku Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ineke Bussemaker, akitia saini kwa upande wa benki hiyo.
Mkataba huo unaendeleza ndoa ya misimu minne, tokea NMB ianze kuidhamini Azam FC mwaka 2014 ilipoibuka mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), ambapo hii ni mara ya tatu wanarefusha ushirikiano huo na Mabingwa hao mara mbili mfululizo wa Kombe la Mapinduzi.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Azam FC, Mohamed, aliishukuru NMB kwa kuendelea kuwadhamini na kuahidi kuendeleza moto wao wa kutwaa mataji chini ya udhamini wa benki hiyo baada ya kuanza na Mapinduzi Cup msimu huu.
“Tutalipa fadhila za kuaminiwa huku kwa kutwaa taji la VPL, kwa sababu, Azam FC inaamini katika mafanikio kama kichocheo cha kuvutia wadhaamini wengine klabuni Azam Complex, Chamazi, moto wetu wa kutwaa mataji utaendelea kwa kutwaa taji la ligi msimu huu ambalo nalo tutalileta hapa kwa mdhamini wetu mwishoni mwa msimu huu,” alisema.
Naye, Bussemaker, alisema benki yake inajisikia fahari kuwa mdhamini mkuu wa klabu hiyo bora iliyoshamiri mafanikio iliyopata katika kipindi cha miaka 10 ya uwepo wao, ikiwemo minne ya kuidhamini.
“Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza kwa kutwaa taji la Mapinduzi Cup 2018 kwa mara ya pili mfululizo, leo tunaongeza mkataba wa udhamini na Azam FC, ambao naamini utaongeza sana maendeleo yao ya sasa ya kukuza vipaji katika klabu yao na kuhakikisha wanakuwa kwenye nafasi yao kama klabu kubwa Tanzania na Afrika kwa ujumla.
“Kwa miaka minne sasa, tumekuwa wadhamini wakuu wa Azam FC na tumeona mafanikio makubwa kwenye klabu na tunayofuraha kuendelea kushirikiana na Azam FC, kupitia mkataba huu, Benki ya NMB tutaendelea kama wadhamini wakuu wa klabu,” alisema.
Bussemaker alisema kuwa kupitia vipengele vya mkataba huo, pande zote mbili wamekubaliana kukuza na kuendeleza soka kwa faida ya pamoja (Azam FC na NMB) na kutumia soka kama gari la kuimarisha mahusiano yao pamoja na ushirikiano.