AFYA za mamilioni ya Watanzania wanaotumia vinywaji vya aina ya soda ipo hatarini, baada ya kugunduliwa uwepo wa chembechembe zenye kemikali za sumu ndani ya vinywaji hivyo, MTANZANIA Jumatano linaripoti.

Utafiti uliofanywa na Muungano wa Waandishi wa Habari za Uchunguzi Tanzania (Investigative Journalists Union of Tanzania- IJUTA) pamoja na tafiti zilizofanywa na wataalamu waliobobea katika afya ya umma duniani, umebaini kuwa vinywaji baridi aina ya soda ni hatari kuliko utumiaji wa sigara inayosababisha maradhi ya kansa katika mwili wa binadamu.

Kwa mujibu wa utafiti wa wanasayansi mbalimbali duniani, yapo madhara makubwa ya utumiaji wa vinywaji vya aina ya soda katika mwili wa binadamu.

Utafiti huo unaonyesha kuwa zipo sababu nane kuu zinazokiweka kinywaji aina ya soda kwenye kundi la vinywaji vyenye sumu ambavyo havifai kwa matumizi ya binadamu.

IJUTA imebaini kuwa makampuni makubwa yanayotengeneza vinywaji baridi aina ya soda yanatumia mabilioni ya dola kila mwaka kujitangaza na kutoa misaada ya kijamii kutokana na mauzo yake, bila kutaja madhara ya vinywaji hivyo kwa binadamu.

Kwamba matangazo hayo yanayogharimu mamilioni ya fedha ndiyo yanayokifanya kinywaji hicho kuwa maarufu zaidi duniani, licha ya kuwa na madhara makubwa katika mwili wa binadamu.

Aidha, utafiti huo unaonyesha kuwa umaarufu mwingine wa kinywaji aina ya soda ni utamu wa kupindukia ulio ndani ya soda.

Utafiti wa IJUTA unaonyesha kuwa utamu wa kupindukia iliomo ndani ya soda unawapumbaza wanywaji ili wasisikie ladha kali ya asidi iliyomo ndani ya soda.

IJUTA imegundua kuwa kiwango cha asidi kilicho ndani ya soda hakiwekwi wazi kwa walaji kwa sababu ya kuhofia kuwa wakibaini wataacha kikutumia kinywaji hicho.

Inaelezwa pia kuwa madini ya cola yaliyo ndani ya soda yana kilevi aina kafein kinachomteka mnywaji kuwa teja wa kinywaji hicho.

Tafiti za kitaalamu zimeonyesha kuwa soda inahusishwa na matatizo mengi ya kiafya kwa watoto na watu wazima, yakiwemo matatizo ya kuongezeka unene kupita kiasi, ugonjwa wa ini na mengineyo.

Utafiti uliofanywa nchini Marekani unaonyesha kuwa soda huwekewa ‘fructose’ (sukari) nyingi kupitia mfumo wa sirapu (fructose corn syrup) ambayo inaongoza kwa kusababisha magonjwa ya unene, kisukari, ugonjwa wa moyo na magonjwa mengine sugu yanayowakabili Wamarekani wengi hivi sasa na dunia kwa ujumla.

Dk. Mercola, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya lishe asilia na tiba mbadala nchini Marekani, amekaririwa na tafiti mbalimbali zilizofanyika nchini humo akieleza kuwa kinywaji aina ya soda ni hatari kwa binadamu, sawa na mtu anayevuta sigara au zaidi, jambo alilosisitiza kuwa siyo la kutia chumvi, bali ukweli halisi.

Watumiaji wa vinywaji aina ya soda wanaelezwa kuwa wamekuwa wakinywa kiasi kikubwa cha kaboni, kafeini (dawa ya kulevya), sukari ya kupundukia na asidi kali ambayo huvuruga afya ya mtumiaji kwa kiwango cha juu.

Soda pia imebainika kutokuwa na lishe ya aina yoyote zaidi ya maji na sukari.

Uchunguzi wa IJUTA na utafiti ya wanasayansi mbalimbali duniani, umeonyesha kuwa watu wengi hawajui kuwa unywaji wa soda huwaongezea kiasi kikubwa cha madini joto.

Chupa moja ya soda yenye ujazo wa mililita 330 husababisha unene kwa kiwango cha paundi moja kwa mwezi.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Kisukari Tanzania (TDA), Ramadhan Mongi, amepata kukaririwa na vyombo vya habari hapa nchini akieleza kuwa ugonjwa wa kisukari Tanzania umeongezeka mara sita katika siku za hivi karibuni.

Alisema miaka kumi iliyopita, hali ya kisukari ilikuwa asilimia tatu (3), lakini katika miaka ya karibuni umeongezeka mara sita.

“Tunastahili kuongeza jitihada ya kupambana na gonjwa hili la kisukari kwa gharama zote kwa sababu kisukari ni moja ya magonjwa manne yanayomaliza Watanzania,” alisema.

Utafiti uliofanyika Mkoa wa Dar es Salaam ulibaini kwamba kati ya watu watano waathirika wa kisukari, mmoja tu ndiyo hupata matibabu ya serikali.

Unywaji kwa mpigo wa kabohaidrets iliyo na sukari nyingi kwenye soda hudhoofisha seli zinazozalisha vimeng’enya tofauti na vyakula vingine na pia imebainika kuwa sukari ikiingia kwa wepesi kwenye mzunguko wa damu husababisha kongosho kuzalisha vimeng’enya vingi mwilini.

Uchunguzi wa kitabibu katika Hospitali ya wanawake ya Boston nchini Marekani na katika Chuo cha Kitabibu cha Harvard umeonyesha wanawake 51,000 hawakuwa na kisukari mwanzoni mwaka wa 1991, lakini miezi minane baadaye wanawake 741 waligundulika na kisukari.

Ripoti ya utafiti huo ilionyesha kuwa wanawake waliokuwa wakitumia kinywaji aina ya soda moja ama mbili kwa siku waliongezeka uzito maradufu na walikuwa hatarini kupata ugonjwa wa kisukari.

Pia ilionyesha kuwa soda hudhoofisha mifupa na husababisha hali ya mifupa kupuputika, hali inayomuweka mtumiaji kuwa katika hatari ya kuvunjika mifupa kirahisi.

Madhara mengine yaliyobainika kusababishwa na unywaji soda ni kupukutika kwa meno na ama kuoza. Pia soda husababisha matatizo ya figo.

Soda yenye chembe ya cola husababisha figo kuwa na mawe kwa sababu ya asidi na kemikali mbalimbali zinazofichwa vipimo vyake kwa walaji.

Madaktari bingwa wa wanamichezo wanaeleza madhara yanayosababishwa na soda mwilini kuwa ni pamoja na shinikizo la damu, uharibifu wa ini, huvurugu mfumo wa kumeng’enya chakula tumboni kutokana asidi ya kiwango cha juu iliyo kwenye soda.

Wanashauri kuwa soda haistahili kutumika kama kishawishi kwenye mchezo, kwa sababu ina madhara makubwa kwa wanamichezo kwa sababu hunyonya maji kwenye mwili na kudhoofisha mwili.

Wakati utafiti huo ukidhihirisha hayo, Taasisi ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imeshindwa kutoa tamko lolote kuhusu utafiti huo, hata baada ya kupelekewa maswali kwa maandishi yanayoomba ufafanuzi wa ubora wa vinywaji vya soda katika mwili wa binadamu.

Soda yapigwa marufuku Ughaibuni
Jumatano, Mei 15, 2013 05:22 Na Fred Okoth

  • Yakatazwa shuleni, watoto chini ya miaka 12
  • Sasa yabainika kuwa ina sumu inayoua taratibu
  • Yagundulika kupumbaza na kusababisha uteja 


SIKU chache baada ya gazeti hili kuripoti madhara yanayosababishwa na kinywaji aina ya soda, katika utafiti wake gazeti hili limebaini mengine mapya.

Kwa mujibu wa utafiti huo, imebainika kuwa soda imepigwa marufuku kutumiwa na watoto walio na umri chini ya miaka 12 na walio shuleni katika baadhi ya mataifa ya Ulaya na Marekani, kutokana na madhara ya kiafya yanayosababishwa na kinywaji hicho.

Taarifa zilizotolewa na Shirika la Habari la The Press Television Technology Advertising and Branding (Adweek) zinazonukuu taarifa ya kampuni moja kubwa duniani inayozalisha kinywaji aina ya soda, imeamua kupambana na unene (obesity), unaosababishwa na unywaji wa soda kwa kuondoa matangazo ya vinywaji vyake kwenye vyombo vya habari.

Kampuni hiyo kupitia taarifa yake hiyo iliyotolewa katika moja ya sherehe zake, ilieleza kuwa lengo la kuondoa matangazo hayo ni kuwanusuru watoto wadogo na matumizi ya vinywaji aina ya soda vilivyobainika kuwa na madhara katika mwili wa binadamu.

Nchini Marekani, tayari imekwishapitishwa sheria inayokataza watoto walio na umri wa chini ya miaka 12, kunywa kinywaji aina ya soda.

Mwenyekiti wa Kampuni hiyo, alieleza kuwa mipango ya mbeleni ya kampuni yake ni kutengeneza kinywaji hicho kikiwa na kiwango kidogo cha Kalori na kubuni kinywaji cha aina hiyo ambacho kitakuwa hakina Kalori.

Alisema mipango hiyo itatekelezwa duniani kote ambako kinywaji cha aina ya soda kinatengenezwa na nchini Marekani tayari imekwishaanza kutekelezwa.

Aidha, Kampuni hiyo imeahidi kuweka wazi virutubisho vyote vinavyotumika kutengeneza bidhaa zake na kuahidi kutoa misaada ya hali na mali kwa nchi zote 200 duniani ambako kinywaji cha soda kinauzwa.

Mbali na Marekani, kinywaji cha aina ya Soda kimekwishapigwa marufuku shuleni katika nchi za Uingereza, Ufaransa na katika majimbo ya Los Angeles, Philadelphia na Miami nchini Marekani na kwa watu wazima matumizi yake yanaelekezwa kuwa ya kiwango kidogo sana.

Vyombo vya habari vya nchini New Zealand, mwezi Machi mwaka huu viliripoti kuwa mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Natasha Harris (31), alifariki kutokana na unywaji wa soda nyingi.

Shirika la habari la AFP la Ufaransa, liliripoti tukio hilo kwa kueleza kuwa Natasha alikuwa akinywa soda nyingi kila siku, jambo ambalo liligeuka kuwa sehemu ya maisha yake kwa kipindi cha miaka mingi.

Kwamba familia ilikuwa ikimuita teja wa soda, baada ya meno yake kuoza kwa sababu ya kunywa soda, alijifungua mtoto ambaye hakuwa na fizi jambo ambalo liligundulika baadaye kuwa lilisababishwa na matumizi makubwa ya kinywaji hicho.

“Tumegundua kwamba, kwa kuzingatia ushahidi uliopo, kama sio unywaji wa soda uliopitiliza, Natasha Harris asingekufa katika muda ule na katika hali alivyokufa

“Ripoti ya Daktari aliyechunguza maiti yake (Pathologia), iligundua kwamba ini lake lilipanuka sana, likawa na mrundiko mkubwa wa mafuta kutokana na kula sukari kwa wingi. Kuwepo kwa madini aina ya ‘potasiam’ kwa kiwango kidogo sana kwenye damu yake, pia kulitokana na unywaji wa soda.” Taarifa ya kitabibu katika Hospitali aliyofia nchini New Zealand ilieleza.

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za kisayansi zilizo kwenye mitandao ya wanasayansi waliobobea duniani, unywaji wa soda humpumbaza mtumiaji na kumsahaulisha kula vyakula vyenye madini muhimu mwilini.

Moja ya andishi linalotahadharisha utumiaji wa kinywaji cha soda na kukitaja kuwa cha hatari kwa matumuzi ya binadamu, ni Jack Winkler, Profesa wa sera za lishe katika Chuo Kikuu cha Metropolitan nchini London, linaloeleza kuwa Soda ni bidhaa ya kishetani inayoua binadamu taratibu baada ya kinywaji hicho kumzalishia magonjwa mengi mwilini yanayomfanya kuwa tegemezi wa dawa.

Wakati msomi huyo akieleza hayo katika utafiti wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Dk. Raymond Wigenge, amelieleza gazeti hili soda siyo kinywaji hatari kwa matumizi ya binadamu kwa sababu kinatumiwa na mamilioni ya watu duniani kote.

Akizungumza na MTANZANIA Jumatano ofisini kwake wiki iliyopita baada ya kutoa ufafanuzi kuhusu madhara yanayosababishwa na kinywaji aina ya soda katika mwili wa binadamu, Dk. Wigenge alisema pamoja na changamoto zilizopo katika kinywaji hicho, taasisi yake haipingi uwepo wa kinywaji hicho sokoni.

“Soda haina shida kwa binadamu na hata mkiendelea kuandika suala hili, sisi tutaendelea kuueleza umma kwamba waendelee kupata kinywaji, hivyo kama ambavyo tumekuwa tukifanya,” alisema.

Alipoulizwa kama anakubaliana na tafiti za wanasayansi bingwa wa magonjwa ya binadamu walioeleza katika tafiti zao kuwa unywaji wa soda una madhara katika mwili wa binadamu, alisema hizo ni changamoto za kawaida, kwa sababu madhara yaliyomo kwenye soda hayamuathiri mtu mara moja bali huchukua muda mrefu.

Wakati Dk. Wigenge akieleza msimamo wake kuhusu kinywaji aina ya soda, nchini Mexico, taasisi ya El Poder del Consumidor inayojihusisha na kutetea walaji, inashinikiza Serikali ya nchi hiyo kuzilazimisha kampuni za soda kuorodhesha madini na chembechembe zote za kemikali zinazotumika kutengeneza kinywaji hicho.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Alejandro Calvillo, amekaririwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo akieleza kuwa unywaji wa soda ni hatari na hilo limethibitishwa na wataalamu wa afya duniani kuwa soda ni sumu mbaya, inauwa taratibu.

Tafiti mbalimbali za wanasayansi zinaeleza kuwa soda ina asidi aina ya ‘phosphoric’ yenye uwezo wa kuvuruga madini ya ‘calcium’ yaliyoko mwilini na kusababisha mifupa na meno kudhoofika.

Aidha, asidi aina ya ‘phosphoric’ huvuruga asidi aina ya ‘hydrochloric’ iliyo tumboni mwa binadamu na hivyo kuharibu mfumo wa kusaga chakula.

Viwanda vya soda ndio watumiaji wakubwa wa sukari na wanasayansi wanasema sukari hupandisha kiwango cha ‘insulin’ ambayo husababisha kasi ya mzunguko wa damu, ugonjwa wa moyo, kupanda kwa ‘Cholesterol, kisukari, kuzeeka mapema, ongezeko la uzito na maradhi mengine.

Aidha inadaiwa kuwa viwanda vya soda pia hutumia dawa ya kulevya aina ya kafeini. Wataalamu wanasema vinywaji vyenye kafeini, husababisha kupanda kwa mapigo ya moyo, kasi ya mzunguko wa damu na matatizo ya kizazi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: