MKUU wa Wilaya ya Rombo, Agness Hokororo ameagiza kufungwa mara moja kwa akaunti maalumu ya kibenki ya halmashauri ya wilaya hiyo ambayo ilikuwa ikitumika kukusanya na kuhifadhi michango ya kugharamia chakula cha wanafunzi shuleni.

Hokororo alitoa amri hiyo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Magreth John, wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Wilaya hiyo.

“Nyie madiwani mnayo nafasi kubwa ya kusimamia pia agizo la Rais John Magufuli la kusitisha michango shuleni, lakini pia DED (Mkurugenzi Mtendaji) hakikisha unasimamisha akaunti iliyokuwa ikitumika kwa ajili ya michango shuleni,” aliagiza.

Januari 17, mwaka huu, Rais John Magufuli alipiga marufuku michango yote katika shule za sekondari na msingi huku akiagiza kuchukuliwa hatua viongozi na watendaji ambao watatoza michango hiyo kinyume na miongozo uliotolewa na serikali wa utoaji wa elimu bure.

Rais Magufuli alisema kama kutakuwapo na mchango wowote wa mzazi ambaye atajisikia kuchangia jambo lolote kuhusu masuala ya shule, basi fedha hizo zipelekwe kwa mkurugenzi wa halmashauri na si kushikwa na mwalimu yoyote yule.

Kumekuwa na mtindo wa kuwarudisha nyumbani baadhi ya wanafunzi katika shule za umma kutokana na kushindwa kutoa michango ambayo ipo nje ya utaratibu wa ada, hali iliyomkera Rais Magufuli na kuingilia kati suala hilo.

Michango katika shule ilihusu kusaidia upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi, ujenzi wa uzio, masomo ya ziada na ulinzi, miongoni mwa sababu mbalimbali.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: