ACT Wazalendo kimetofautiana na (CHADEMA) kuhusu kushiriki katika uchaguzi wa marudio ambao unatarajiwa kufanyika Februari 17, 2018 katika jimbo la Kinondoni na Siha. ACT Wazalendo wanasema kushiriki uchaguzi huo ni kuhalalisha mchakato haramu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu Katibu Mkuu (Bara) ACT Wazalendo ndugu Msafiri Mtemelwa amesema kuwa uwanja wa Demokrasia nchini bado si sawa na kuwa kushiriki uchaguzi huo ni kuhalalisha mchakato haramu, hivyo wao ACT Wazalendo hawapo tayari kuhalalisha jambo.
"Chama cha ACT Wazalendo kimeona ni jambo muafaka kutoa ufafanuzi kwa wanachama wake na wananchi kwa ujumla kuhusu nafasi na msimamo wake kwenye uchaguzi wa marudio kwenye Majimbo ya Kinondoni na Siha na Kata tisa uliopangwa kufanyika tarehe 17 Februari, 2018.
"Ikumbukwe kuwa Kamati ya Uongozi ya ACT Wazalendo iliyoketi tarehe 8 Novemba 2017 iliamua kusitisha ushiriki wa Chama chetu kwenye uchaguzi wa tarehe 13 Januari 2018 na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu kufanya tathmini na uamuzi juu ya Chama kushiriki kwenye chaguzi za marudio.
"Ni Jambo la kiukombozi kwamba baadhi ya vyama vya upinzani navyo vilichukua mkondo huo wa kugomea uchaguzi"
Mtemelwa aliendelea kusisitia kuwa wao waliamua kujitoa kwenye uchaguzi huo kutokana na vyombo vya dola kuingilia mchakato wa uchaguzi na kulazimisha ushindi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
"Hata hivyo tunatambua kuwa kutoshiriki chaguzi tu haitoshi kwani haijibu swali la nini kinafuata baada ya kususia. Chama chetu pia kinatambua kuwa Chama tawala kinaweza kufurahia kususiwa na kuna uwezekano mkubwa wa kuendelea kubinya demokrasia ili vyama vya upinzani viendelee kususia chaguzi zinazokuja.
"Kamati Kuu imeuagiza Uongozi wa Taifa wa Chama kuwafikia wadau wote wa demokrasia nchini na kuweka mikakati ya pamoja ya hatua za ziada za kuchukua ili kuboresha mazingira ya chaguzi za haki nchini kwetu pamoja na kuweka shinikizo kubwa kwa serikali kufanya mabadiliko muhimu ya kisheria, kiutendaji na kikatiba ili kuweka sawa uwanja wa mapambano ya kidemokrasia"
Kutokana na mambo hayo ACT Wazalendo wakaweka msimamo wao
"Hivyobasi, tunapenda kuweka bayana kwamba Chama chetu hakitoshiriki kwenye uchaguzi wa marudio wa tarehe 17 Februari kwenye Majimbo ya Kinondoni, Siha na udiwani kwenye Kata tisa.
"Msimamo huu unatokana na ukweli kwamba sababu zilizolalamikiwa kwenye uchaguzi wa 13 Januari, 2018 hazijabadilika kwa sehemu kubwa. Mageuzi madogo yaliyofanywa na Tume ni kauli yao kuwataka Wakuu wa Wilaya kuacha kuingilia uchaguzi. Hili ni tone dogo katika malalamiko ya vyama vya upinzani dhidi ya Tume" alisema Mtemelwa
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo chenyewe kimetangaza kushiriki uchaguzi huo wa marudio katika majimbo mawili Kinondoni na Siha na tayari wameshachukua fomu Tume ya Uchaguzi na kuzirudisha.
Post A Comment: