Golikipa wa Singida United na timu ya taifa ya Tanzania Peter Manyika Jr amefunguka kuhusu mkasa wake wa kukaa benchi kwa muda mrefu akiwa Simba hadi kuamua kuachana na klabu hiyo baada ya mkataba wake kumalizika.
“Kuna vitu vidogovidogo ambavyo vilikuwa vinaingiliana kati ya kazi na maisha ya kawaida, hiyo ndio ilinigharimu. Sisi vijana mambo mawili matatu yakitokea lazima yakuvuruge. Nashukuru Mungu kichwa changu kimetulia nimepata ushauri mpya, nimerudi kwenye njia ambayo nilikuwa nahisi itanifikisha pale napohitaji kufika,”-Peter Manyika Jr via TBC.
“Muhimu ni kuelewa umekosea wapi katika kazi yako au maisha na ukijipanga tena, ukijipanga tena na kujituma  na ukitumia akili yako vizuri basi utarudi kwenye njia yako ambayo wewe unaihitaji kurudi.”
Manyika Jr ameidaikia Singida United mechi zote (11) hadi sasa za msimu huu na kuisaidia timu hiyo iliyorejea VPL kupata pointi 20 na kushika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kuu ikiwa ni tofauti ya pointi tatu na vinara wanaoongoza ligi hiyo.
Katika mechi 11 ambazo Manyika Jr amesimama golini, Singida United imepoteza mchezo mmoja (Mwadui 2-1 Singida United) huku akiwa hajaruhusu kufungwa goli katika mechi saba, amefungwa magoli matano pekee katika mechi zote 11.
Kwa sasa Manyika Jr yupo nchini Kenya akikitumikia kikosi cha Tanzania bara (Kilimanjaro Stars) kwenye michuano ya CECAFA Challenge Cup 2017.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: