Kamanda wa polisi Mkoani Pwani ,Jonathan Shanna mwenye kifimbo akiwa pamoja na askari wa polisi Mkoani hapo ,wakati wakijifua na mazoezi kuelekea kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka,viwanja vya Mailmoja Kibaha.
Picha na Mwamvua Mwinyi
………………..
23,Des
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
JESHI la polisi Mkoani Pwani limetoa onyo kali kwa wale wenye nia ya kutenda uhalifu, katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye sikukuu za mwisho wa mwaka ,wabadili mawazo yao kabla ya hatari kwani jeshi hilo limejipanga kikamilifu kulinda raia na mali zake.
Aidha jeshi hilo limewataadharisha watu wote wanaokwenda ndani ya Mkoa huo hususan kwenye fukwe za bahari ya Hindi zilipo kwenye wilaya ya Bagamoyo ,kuwa wastaarabu na kutii sheria za nchi na watakaokiuka hawatakuwa na muhali nao ili iwe mfano kwa wengine.
Kamanda wa polisi Mkoani Pwani (ACP)Jonathan Shanna ,alitoa wito huo viwanja vya Mailmoja Kibaha wakati akizungumza na waandishi wa habari na baadhi ya wananchi waliojitokeza kujionea askari waliokuwa wakifanya mazoezi ,kuelekea kipindi cha sikukuu ya X-Mas na mwaka mpya.
Alitoa wito, kwa wenye kumbi za starehe kuzingatia sheria za usalama kwa kutojaza idadi kubwa ya watu kwenye kumbi zao na wale watakaokaidi watakiona .
Pamoja na hayo ,kamanda Shanna aliwataka wananchi kuhakikisha wanapotoka majumbani mwao ,wasitoke wote na waache walinzi kwenye nyumba zao.
Aliwaasa pia wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwaachia watoto wao kwenda kwenye shamrashamra za sikukuu pasipo kuwa na wangalizi ili kuepuka upotevu wa watoto.
Kamanda Shanna alieleza kuwa ,askari wa jeshi hilo Mkoa wapo kamili ,shupavu na majasiri katika kuzuia matukio ya uhalifu kupitia mbinu za kimedani walizowapatia .
“Sisi jeshi la polisi Mkoa tumejipanga katika kuhakikisha usalama ndani ya mkoa wetu unakuwa ni jambo endelevu sio wakati huu wa sikukuu pekee ,ili kuunga mkono kauli mbiu ya serikali yetu ya Tanzania ya na Tanzania yenye amani’alisema Kamanda Shanna.
Kamanda huyo Mkoani hapo alielezea kwamba,usalama ni bidhaa adimu ,usalama unapotoweka watu huweza kukimbia nchi yao na kuitwa walimbizi katika nchi nyingine .
Hivyo ,Kamanda Shanna alisema watahakikisha wanatunza tunu ya amani iliyopo ili kuweza kuwavutia wawekezaji kuendelea kuwekeza katika Mkoa huo.
Jeshi hilo limeahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakaojaribu kuchezea usalama uliopo mkoani humo .
Katika hatua nyingine aliwashukuru waandishi wa habari mkoani hapo ,kwa ushirikiano wanaouonyesha kwa jeshi hilo .
Kamanda Shanna alibainisha ,ushirikiano huo umemsaidia kwa kiwango kikubwa katika mapambano ya kuzuia na kutanzua uhalifu.
Aliwaomba ushirikiano uendelee ili kuhabarisha umma juu ya matukio yanayotokea na mikakati wanayoendelea nayo
Post A Comment: