Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema ili shule isajiliwe lazima iwe imekidhi vigezo ikiwa ni pamoja na kuwa na madarasa ya kutosha, nyumba za walimu, ofisi za walimu, matundu ya vyoo, pamoja na maabara endapo shule itakuwa ni ya Sekondari.
Waziri Ndalichako ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa halmashauri ya Mbulu iliyopo mkoani Manyara ambapo amesema ni kweli serikali inahitaji ziwepo shule nyingi ambazo zinavigezo, siyo kuwa na shule ambazo hazinavigezo.
"Shule za nyasi katika Serikali hii ya awamu ya Tano zitabaki kuwa historia kwa kuwa serikali inajenga na kuboresha miundombinu ya kujifunzia na ile ya kufundishia, sasa ili shule isajiliwe lazima iwe imekidhi vigezo siyo bora shule bali tunahitaji shule zilizobora na zenye viwango vinavyokubakika" amesema Waziri Ndalichako.
Waziri Ndalichako amesema kazi ya usajili ni nyepesi sana ambayo haichukui muda mrefu endapo vigezo vinakuwa vimetimia, lakini kazi kubwa ni kuhakikisha miundombinu bora inayokubalika inakuwepo ili shule iweze kusajiliwa.
Hivyo amewasihi wadau wote wa Elimu kuhakikisha shule zinapojengwa zinazingatia na kukidhi vigezo kabla ya kusajiliwa.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
19/11/2017
Post A Comment: