WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa wilaya ya Ruangwa wapande miche mipya ya mikorosho ili waweze kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Ametoa wito huo jana (Jumapili, Novemba 5, 2017) wakati akizungumza na wakazi wa kata za Mbekenyera na kata jirani kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Mbekenyera, wilayani Ruangwa mkoani Lindi.
“Mkuu wa Mkoa ameelezea nia ya mkoa wake kutoa miche mipya. Ninawasihi, mfuate maelekezo hayo. Ili uweze kuendelea kuvuna, itabidi ukate mikorosho ya zamani kwa awamu na upande mipya. Hii itakusaidia kuendelea kuvuna wakati ile mingine ikikua,” alisema.
“Wenzetu wa Nanyamba waliijua siri hii mapema, wakapanda miche mipya na sasa hivi kila mkorosho unawapatia siyo chini ya kilo 12,” aliongeza.
Akizungumzia zao la ufuta, Waziri Mkuu alisema msimu ujao itabidi zao hilo lianze kuuzwa kwa kutumia mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani na akawataka wakazi hao wajiandikishe pindi tu msimu ukianza, kila mmoja na kiasi ambacho amevuna.
“Siku ya mnada, kila ghala itabidi waseme bei yao na wana tani ngapi walizokusanya. Mnunuzi akija atasema anataka tani ngapi. Kupitia mfumo wa mnada, ndiyo mkulima ananufaika,” alisisitiza.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaalika wakazi wa Mbekenyera na kata za jirani washiriki kwa wingi kwenye sherehe za Maulid zinazotarajiwa kufanyika kitaifa wilayani Ruangwa Desemba mosi kwa mkesha wa Maulid na kufuatiwa na Baraza la Maulid litakalofanyika Desemba 2, mwaka huu.
“BAKWATA ilizoea kuadhimisha sherehe hizi Dar es Salaam au makao makuu ya mkoa. Mwaka huu ndiyo imeanza kwenda wilayani, kwa hiyo tunapaswa kujitokeza kwa wingi ili kuifanikisha siku hii. Sote tuje Ruangwa ili kuhudhuria mkesha wa Maulid na kesho yake tunaunganisha na Baraza la Maulid, chai na chakula vitakuwepo,” alisema.
Mapema, Mkuu wa mkoa huo, Bw. Godfrey Zambi alisema mkoa huo umejipanga kuzalisha miche milioni moja kwa kila Halmashauri katika mkoa huo na kwamba miche hiyo inapaswa igawiwe bure.
Waziri Mkuu amerejea Dodoma leo asubuhi kuendelea na vikao vya Bunge vinavyotarajiwa kuanza kesho (Jumanne, Novemba 7, 2017).
Post A Comment: