Na Ngariba Mkuu
Machame, Hai Kilimanjaro
15/11/2017
*Salamu* , nimeona niseme Machame nikiwa Mapumzikoni kijijini.
*CHADEMA* kama kawaida wameendeleza tabia yao ya kushangilia kumpokea Mwanachama wa *CCM* anayehamia kwao kama shujaa na kumponda MWANA CHADEMA anayeondoka kama msaliti.
Imefikia mahali *Godbless Lema* anadiriki kuandika kumfananisha *Lawrence Masha* kama 'mvulana' na wao kama 'wanaume' wanaoendelea na mapambano.
Ni wakati sasa *CHADEMA* wakaacha kufukia kichwa kwenye mchanga na kujidai kila kitu kiko sawa ndani ya chama chao. Wataweza kufanya hivyo kama viongozo wake wakibadilika.
Kitendo cha CHADEMA kumpokea *Lazaro Nyalandu* na kuanza kumtetea kwa yale yote ambayo walimsema huko nyuma ni jambo la ajabu ingawaje lilitegemewa. Walifanya hivyo hivyo wakati wa *Edward Lowassa* na *Fredrick* *Sumaye* .
Ni wazi kabisa kwa *CHADEMA* ukiwa upande wao basi uchafu wako wote ni usafi. Watatumia kila nafasi kuhakikisha unasafishika kwenye macho ya wafuasi wao. Ukiondoka kwao wewe ni msaliti na umenunuliwa na *CCM* ! Nyalandu leo hii ni shujaa!
*CHADEMA* ukiwa na uwezo wa kifedha wewe ni dhahabu. Ukiwa hohehahe basi sahau mchango wako kutambuliwa na kuthaminiwa na viongozi wa CHADEMA.
*Ghafla* CHADEMA wamesahau mchango wa Masha kwenye uchaguzi mkuu. Wamesahau kwamba ni 'mvulana' huyo huyo ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na mfuasi muaminifu wa Edward Lowassa alithubutu kujitoa CCM na kujiunga nao. Aliwasaidia kwenye kampeni ambazo zimewapatia wabunge na madiwani nchi nzima! Wakati huo Masha hakuwa mvulana??
*CHADEMA* wamesahau kwamba Masha alipopata kesi kwa kufanya mkutano wa kampeni ndani ya Kambi ya Wakimbizi Mpanda walimtelekeza bila msaada *WOWOTE* .
*Masha* alisimamia kesi yake pamoja na viongozi wa Wilaya wa Mpanda mwenyewe na kwa gharama zake mpaka akashinda. Hili hawalioni. Halina maana yoyote kwao.
*CHADEMA* wamesahau kwamba Masha alipopata kesi baada ya kwenda kituo cha polisi Oysterbay kuwatetea wafuasi wao walimuachia hiyo kesi apambane nayo. Wamesahau kwamba Wakili wa Chama alitaka alipwe fee kumtetea Masha! Wanasahau kwamba ' *mvulana* ' Masha alilala magereza kwa kutetea haki za wafuasi wao!
*CHADEMA* wamesahau kwamba wakati Masha alipoamua kugombea Uraisi wa Chama cha Wanasheria walimruhusu Lissu achuane nae. Jitihada za Masha kwamba Lissu ajitoe ili wasigawane kura hazikuwa na maana yoyote kwa CHADEMA.
*Lissu* ambaye ni Mbunge, Mnadhimu, Mwanasheria Mkuu wa Chama, Mjumbe wa Kamati Kuu na sasa Raisi wa TLS ni muhimu na wa maana sana kuliko mvulana Masha.
*CHADEMA* wamesahau kwamba wakati Masha anagombea ubunge wa EALA walimuwekea Wenje makusudi wakijua kuwa wote hawatapita! Hata walipoona kwamba lazima kuwe na mgombea mwanamke hawakuona sababu ya kufanya lolote. Mtu yeyote anayeingia kwenye siasa ana malengo binafsi na sio dhambi! Kwa Masha hakuna tofauti.
*CHADEMA* wamesahau kwamba Edward Lowassa na Fredrick Sumaye wamepewa vyeo mara baada ya kujiunga. Kwa nini? Kwa sababu wao wanatokea Kaskazini na wana fedha kuliko Masha? Haya ni mambo ambayo watayapuuza na kuyakalia kimya.
*Wakati* Masha akiwa kwenye Tafakuri kubwa ya Hatma ya Maisha yake kisiasa, endapo ataamua kurudi Chama cha Mapinduzi, Kuna ambao watasema Masha amenunuliwa. Masha ana njaa na hana msimamo.
Hawatakubali kwamba
1. Ni uhuru wake na ndio maana ya demokrasia
2. Wameshindwa kuweka mazingira rafiki ya yeye kufanya siasa na kutoa mchango wake
3. Wamekosa muelekeo kwa kubaki kufanya siasa za matukio.
Wasalamu
Ngariba Mkuu
Machame Hai, Kilimanjaro
15/11/2017
Post A Comment: