Tatizo la maji kwa wakazi wa halmashauri ya Arusha linategemewa
kupungua ifikapo mwaka 2018/19 kwa kuongeza upatikanaji wa maji kwa
wakazi hadi kufikia zaidi ya 80% kutoka asilimia 54.2 za sasa.
.
Hayo yamethibitishwa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack
Kamwele alipokutana na wataalam wasimamizi wa mradi wa maji wa vijiji
vitano halmashauri ya Arusha maarufu kama mradi wa WaterAid
walipokutana kwenye hotel ya Mount Meru jijini Arusha na kuthibitisha
kuwa mkakati wa serikali ni kuhakikisha maji yanapatikana kwa zaidi ya
asilimia 90% .
Waziri Kamwele amethibitisha kutekeleza ahadi yake ya shilingi bilioni
2.3 aliyoitoa mwezi Februari, 2017 akiwa Naibu Waziri wa Maji aliahidi
kutoa kiasi hicho cha fedha kwa lengo la kupanua mradi wa maji wa
OLMULO unaohudumia wakazi wa kata za Oljoro na Laroi halmashauri ya
Arusha.
Waziri Kamwele amesema kuwa fedha hizo zitatolewa ndani ya mwaka huu
wa fedha ili huduma ya maji ipatikane umbali usiozidi mita 400 kwa
kila mwananchi ifikapo mwaka 2020.
Hata hivyo Waziri Kamwele ameahidi kutoa fedha nyingine kiasi cha
shilingi bilioni 1 kwa ajili kuendeleza chanzo cha maji cha Emutoto
kilichogundulika wakati wa upembuzi yakinifu wa mradi wa maji wa
vijiji vitano mradi unaotekelezwa na shirika la kimataifa la WaterAid.
Waziri huyo amefikia uamuzio huo wenye lengo la kuongezea nguvu za
upatikanaji wa huduma ya maji kwenye kijiji cha Ilkuroliti na baadhi
ya maeneo ya kata ya Oldonyosambu ambayo licha ya kuwa na uhaba wa
maji wanakabiliwa na tatizo la Floraidi iliyozidi kwenye maji ya eneo
hilo.
Mhandisi wa Maji halmashauri ya Arusha Mhandisi Joyce Bahati amesema
kuwa fedha hizo zitasaidi kuongeza nguvu kwenye mradi wa vijiji vitano
ambao tayari upembuzi yakinifu umekwishafanyika na kuwa ni njia rahisi
ya kuongeza matawi zaidi.
Ameongeza kuwa mradi wa vijiji vitano ulikuwa uwafikie watu elfu
hamsini lakini endapo mradi utaongezeka utaongeza watu zaidi ya elfu
tano wa vijiji vya Ilkuroti na baadhi ya maeneo ya Oldonyosambu.
Aidha Mhandisi Bahati amesema kuwa kuendeleza chanzo cha Emutoto
kitasababisha urahisi wa kuendeleza matawi kwenye vijiji ambavya
havina maji kwa kuelekea ukanda wa Oldonyosambu zaidi.
Mradi wa maji wa vijiji vitano umefadhiliwa na shirika la Maendeleo la
Uingereza DFID na kutekelezwa na shirika la WaterAid unategemea
kuhudumia watu elfu hamsini kwenye vijiji vya Lengijave na Olkokola na
vitongoji vya Seuri, Ekenywa na Ngaramtoni kwa gharama ya shilingi
bilioni 4.5 na kutekelezwa ndani ya mwaka mmoja.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: