Na Meitoris Ignatus.
Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanamuhusu kila mtu katika karne hii bila kujali umri, mahali wala muda na kuifanya jamii kujikita kwenye eneo hilo katika sekta zote za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
Teknolojia ya habari na mawasiliano ni nyenzo muhimu ya kuwezesha mageuzi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa kutekeleza hilo Serikali kupitia wizara ya Elimu imelazimika kuingiza kwenye mitaala ya elimu kwenye ngazi zote za elimu kuanzia shule za msingi mpaka elimu ya juu.
Halmashauri ya Arusha haiko nyuma katika matumizi ya teknolojia ya mawasiliano na imeweka kipaumbele katika kuhakikisha jamii inatumia teknolojia ya mawasiliano katika sekta zote pamoja na kuanza mkakati wa kuhakikisha wanafunzi wa shule za sekondari wanasoma somo la TEHAMA kwa nadharia na vitendo.
Aidha halmashauri kwa kushirikiana na shirika la International Education Outreach Incorporated wamefanikiwa kuwezesha miundo mbinu ya madarasa na vifaa vya TEHAMA kwenye shule za sekondari.
Afisa TEHAMA na Mratibu wa mradi wa Teknolojia ya Habari shule za sekondari ndugu halmashauri ya Arusha ndugu David Nyangaka amesema kuwa mpaka sasa jumla ya shule 10 za sekondari zina miundombinu na vifaa vya kufundishia somo la TEHAMA ikiwa ni pamoja na Kompyuta vifaa vyake vyote.
Ameongeza kuwa vifaa hivyo vya TEHAMA vinafadhiliwa na shirika la RENEAL la nchini Uingereza ambapo wametoa jumla ya kompyuta 250 kwa shule za sekondari 10 za Mlangarini, Mukulat, Ilkiding'a, Mwandet, Enyoito, Ilboru, Mringa, Oldadai, Mateves na Nduruma.
Nyangaka amefafanua kuwa somo la TEHAMA shuleni ni muhimu kwa kuwawezesha wanafunzi kuendana na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia yaliyoifanya dunia kuwa kijiji kimoja.
"Tumeamua kutekeleza sera hii kwa kasi kwa kwa kushirikiana na wadau wetu wa RENEAL ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa matumizi ya teknolojia ya mawasiliano.
Ameongeza kuwa somo hilo litawaongezea na kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujiamini na kuwa bora kimasomo na kuendana na karne hii ya sayansi na teknolojia.
Shule ya Sekondari ya Mringa ni moja ya shule zinazofundisha somo la TEHAMA mwandishi wa hari hizi amefanikiwa kufika shuleni hapo na kujionea somo hilo la teknolojia ya mawasiliano likifundishwa na kuzungumza na walimu na wanafunzi.
Wanafunzi wa kidato cha pili na cha tano wameeleza kuwa licha ya kujifunza somo la Teknolojia ya habari na mawasiliano lakini pia kompyuta hizo zimewasadia kwa kiwango kikubwa katika masomo mengine kutokana na uhaba mkubwa wa vitabu uliopo shuleni.
Yassir Yusuph mwanafunzi wa kidato cha pili amesema kuwa mradi huu umerahisisha upatikanaji wa matirio ambayo wangehangaika kutafuta kwenye vitabu ambazo ni vichache na havitoshelezi kulingana na idadi yao.
"Tumefurahi sana kwa kujua matumizi ya teknolojia ya mawasiliano kwani imetuwezesha kupata material ya masomo yote kwa urahisi tofouti na kutumia vitabu pamoja na kujisomea mambo mbalimbali yanavyoendelea duniani" amesema Yassir.
Nae Tumaini Ernest wa kidato cha tano amethibitisha kuwa somo la teknolojia ya mawasiliano limewawezesha limewezesha kupandisha kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wengi kutokana na upatikaniji rahisi wa mada za masomo wanayofundishwa.
Ameongeza kuwa somo la teknolojia ya mawasiliano limewaongezea wanafunzi uwezo wa kujiamini kutoka na kuwa na ufahamu wa maarifa mbalimbali ya kimasomo na nje ya kimasomo
"Somo hili limetuongezea kujiamini kwani huwa tunakutanishwa na Shule zingine na kubadilishana mawazo kimasomo jambo linalotufanya kuwa bora katika masomo yetu" amesema Tumaini.
Mwalimu wa taaluma shule ya Sekondari Mringa mwalimu Nampanda Mussa amesema kuwa somo la teknolojia ya mawasilia limesaidia kuinua kiwango cha elimu pamoja na ufaulu shuleni hapo kutokana na urahisi wa upatikanaji wa nyenzo za kujifunzia.
Ameongeza kuwa somo hilo pia limesaidia kuziba pengo la upungufu wa vitabu uliokuwepo shuleni hapo jambo ambalo lilikuwa linapunguza ufanisi wa ufundishaji na ujifunzaji.
"Wanafunzi wako interested kujifunza kwa kutumia Computer, so licha ya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi limeongeza ari ya wanafunzi kujifunza na walimu kufundisha" amesema
Pia Mwalimu wa somo la teknolojia ya mawasiliano Adam Namama amesema kuwa mradi huu umekuwa na faida kubwa kwani umerahisisha mfumo wa elimu na upatikanaji wa silabas ambazo zinapatikana kwenye mfumo ambao umefungwa kwenye kompyuta hizo.
Mwalimu Namama amesema kuwa kwa sasa wana vipindi viwili tu kwa wiki hivyo wanajipanga kuhakikisha kila siku kunakuwa na kipindi.
"Tuna mikakati ya kuhakikisha kuwa somo hili linapata vipindi vingi zaidi kuliko ilivyo sasa ambapo tuna vipindi viwili tu kwa wiki jambo ambalo hutulazimu kutumia muda wa jioni na hata usiku ili kufundisha somo hili" amesema Namama.
Hata hivyo Afisa Elimu Taaluma Idara ya Elimu Sekondari halmashauri ya Arusha mwalimu Charle John amesema kuwa kwa mwaka huu 2017 ni wanafunzi 13 tu wa shule ya sekondari Muklat ndiyo wamefanya mtihani wa taifa wa cha kidato cha nne kwa somo la TEHAMA.
Ametabanaisha kuwa ingawa idadi hiyo ni ndogo lakini pia ni hatua kutokana na muda ambao somo hilo lilipoanza kufundishwa katika shule za halmashauri hiyo.
"Idadi hiyo ni ndogo lakni tunaelekea kwenye mafanikio na tunategemea idadi hiyo kuongezeka kila mwaka na kuongeza usajili wa idadi ya shule kufanya mitihani ya kitaifa" amefafanua.
Hata hivyo Afisa taaluma huyo ameongeza kuwa licha ya mafanikio hayo bado kuna changamoto ya ukosefu wa kompyuta katika shule na baadhi ya shule kutokuwa na umeme .
" Halmashauri ina shule 25 na kati ya hizo shule 10 tu ndio zina vifaa vya kujifunzia somo la TEHAMA bado shule zaidi ya nusu ya shule zetu hazina vifaa hivyo" amesema
Jumla ya kompyuta 177 zinatumika kwenye shule 10 za halmashauri takribani wanafunzi 10,000 wanafundishwa somo la teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Aidha uongozi wa halmashauri unaendelea kuwaomba wadau mbalimbali wa elimun kujitokeza kwa wingi kuchangia upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia soma la teknolojia ya habari na mawasiliano ili somo hilo lifundishwe kuanzia shule za msingi.
Post A Comment: