Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa Changamoto za jamii ni nyingi kuliko mahitaji ya Katiba hivyo suala la katiba sio kipaumbele cha serikali kwa sasa.
Ameyasema hayo leo Bungeni mjini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, ambapo alijibu swali la Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea lililohoji kuwa ‘Serikali ya awamu ya tano imetimiza miaka miwili lakini hakuna jitihada zozote zilizofanywa katika kuendeleza mchakato wa katiba ulioachwa na Serikali ya awamu ya nne.
Aidha, wakati akijibu swali hilo, Majaliwa amefafanua Katiba mpya inahitaji gharama kubwa na Serikali ya Awamu ya Tano imeanza kutatua changamoto za jamii kwanza, ikiwemo mahitaji ya maji, changamoto za elimu, na sekta ya Afya.
“Kila bajeti ina vipaumbele vyake, kwa sasa acha tufanyie kazi vile ambavyo vinasumbua wananchi wengi kwani kipaumbele kikuu ni kuimarisha huduma za jamii hivyo tunasimamia ukusanyaji mapato ili tumalize changamoto hizi na katiba ni muongozo tuu acha tutumie huu uliopo sasa,” amesema Majaliwa.
Hata hivyo, ameongeza kuwa Katiba ni muongozo tu na wakati ukifika serikali yake imemaliza changamoto basi wataanza mchakato huo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment:

Back To Top