KATIBU wa NEC, Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole leo atakuwa LIVE bila chenga katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Kitwiru, Iringa Mjini shughuli itakayohudhuriwa pia na Mbunge wa Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde a.k.a Kibajaji.
Mbali na kumnadi mgombea udiwani wa kata hiyo Baraka Kimata, kiongozi huyo anayefahamika pia kwa ustadi wake wa kujibu hoja mbalimbali za wapinzani wa CCM na serikali yake, atatumia jukwaa la chama hicho kufafanua utekelezaji wa Ilani ya CCM uliofanywa na serikali ya awamu ya tano katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ya Rais Dk John Magufuli.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Iringa Mjini Eddo Bashir ameuambia mtandao huu kwamba mkutano huo unaotarajiwa kuhudhuriwa na mamia ya wafuasi, wapenzi, wapiga kura na wanachama wa chama hicho utaanza saa 8.30 mchana katika uwanja wa kata hiyo.
Bashir alisema Kibajaji anayesifiwa kwa kutumia hoja (Logic) kujibu taarifa mbalimbali za wapinzani wao, atatumia jukwaa hilo kutoa ufafanuzi wa hoja zenye ukakasi zilizotolewa na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika mkutano wao wa uzinduzi wa kinyang’anyiro hicho, uliofanyika jana.
Wakati CCM imemsimamisha Kimata aliyekuwa Diwani wa kata hiyo kupitia Chadema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kabla ya kutimkia CCM hivikaribuni kwasababu ambazo pia zitatolewa katika mkutano wa leo, Chadema wamemsimamisha Bahati Chengula.
Aliwataja wengine watakaopanda katika jukwaa la chama hicho kuwa ni pamoja na wabunge wa viti maalumu, Ritta Kabati na Zainabu Mwamwindi, mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa na viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho
Post A Comment: