Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza wakuu wa wilaya na wakuu wa shule Mkoani humo kumkamata na kuwaweka ndani wazazi na mwanafunzi yeyote wa kike atakayebainika kuwa na mimba hadi hapo watakapomtaja aliyesababisha mimba hiyo. 

Amesema kuwa kumekuwa na tabia ya kumalizana kienyeji huko majumbani na matokea yake watuhumiwa hawafikishwi sehemu husika ili waweze uwajibishwa na hatimae kupunguza kasi hiyo ya mimba kwa wananfunzi. 

“Mwalimu Mkuu unapogundua tu kwamba mwananfunzi ana mimba mweke pembeni ita wazazi wake, washirikishe polisi wawachukue wawekwe ndani kwa muda wa masaa 48, hadi hapo watakapomtaja muhusika wa mimba hiyo, ukifanya hivyo mara kadhaa mabadiliko yatatokea,” Amesisitiza

Ametoa agizo hilo baada ya kusomewa taarifa ya shule ya sekondari Kirando, Wilayani Nkasi wakati alipotembelea kukagua ujenzi wa maabara wa shule hiyo pamoja na na kuongea na wanafunzi, taarifa iliyobainisha kupatikana kwa mimba saba kwa kipindi cha Januari hadi oktoba mwaka huu na kesi zote zipo polisi. 

Halikadhalika alitahadharisha kuwa shule yeyote atakayoitembelea katika ziara yake hiyo ya kujitambulisha katika Halmashauri nne za mkoa huo, ihakikishe inabainisha hatua zilizochukuliwa kwa watuhumiwa na zilipofikia na si kueleza tu idadi ya kesi na kuwepo kwa kesi hizo polisi. 

 Kwa upande wake mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kirando Erneo Mgina amesema kuwa kati ya wanafunzi saba waliopata ujauzito wanafunzi watatu ni wa “A – Level” na wanne ni wa “O – Level” na kueleza kuwa wengi wao hupata mimba wakati wa likizo na huwabaini pale tu wanaporudi shule na kuwapima. 
Share To:

msumbanews

Post A Comment: