Mkutano  wa tisa wa Bunge la 11 utaanza vikao vyake kesho mjini Dodoma  huku kukiwa na hofu ya kusimamishwa kuhudhuria vikao vya chombo hicho cha kutunga sheria kwa wabunge wawili Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) na Saed Kubenea (Chadema).

Katika mkutano uliopita wa chombo hicho cha kutunga sheria, Spika Job Ndugai aliagiza wawili wakamatwe na polisi na kufikishwa mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge akiwatuhumu kwa utovu wa nidhamu.

Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, alifika mbele ya kamati hiyo na kujitetea, lakini kamati hiyo haikufanikiwa kumhoji Kubenea baada ya Mbunge wa Ubungo huyo kufika mbele yake akiwa anasukumwa kwenye kiti cha wagonjwa.

Kubenea anadaiwa kulitumia Kanisa la Ufufuo na Uzima kumtuhumu Spika kusema uongo bungeni kuhusu idadi ya risasi alizopigwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema).

Kwa upande wa Zitto, anadaiwa kumtuhumu Spika kukosea utaratibu alioutumia katika kushughulikia ripoti mbili za uchunguzi wa almasi na tanzanite akidai ripoti zake zilipaswa kujadiliwa bungeni.

Kutokana na tuhuma hizo, kamati hiyo ya bunge inatarajiwa kutoa taarifa yake kuhusu kuhojiwa kwa wabunge hao na hatima yao katika mkutano wa chombo hicho utakaoanza kesho.

Masuala mengine yanayotarajiwa kuwamo katika shughuli za vikao vya mkutano huo ni pamoja na wabunge kujadili na kuishauri serikali kuhusu mapendekezo ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na serikali katika mwaka wa fedha unaofuata.

Kwa mujibu wa kifungu cha 94(1) cha Kanuni za Bunge, chombo hicho katika mkutano wake wa Oktoba - Novemba kwa kila mwaka, kwa siku zisizopungua tano, kinapaswa kukaa kama kamati ya mipango ili kukidhi matakwa ya Ibara ya 63(3)(C) cha Katiba kwa kujadili na kuishauri serikali kuhusu mapendekezo hayo.

Katika mkutano huo, Bunge pia linatarajiwa kupokea, kujadili na kutoa maoni na ushauri kuhusu mwongozo wa kuandaa mpango na bajeti ya serikali.

Kifungu cha 94(2)(b) cha Kanuni za Bunge kinabainisha kuwa Bunge katika mkutano huo litapokea, kujadili na kutoa maoni na ushauri kuhusu vyanzo vya mapato vya serikali na pia litapokea, kujadili na kutoa maoni na ushauri kuhusu mapendekezo ya utekelezaji wa mpango wa serikali na vipaumbele kuhusu mpango huo.

Wabunge watapokea taarifa za utekelezaji wa bajeti ya serikali kwa nusu mwaka kuanzia Julai hadi Novemba.

Katika mkutano huo, Bunge linatarajia kujadili na kupitisha miswada mbalimbali ukiwamo Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Namba 4 wa mwaka 2017, Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano (TTCL) wa mwaka 2017 na Muswada wa Uwakala wa Meli Tanzania.

Bunge pia linatarajiwa kuutumia mkutano huo kutapokea taarifa za utekelezaji wa kamati zake katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2017/18.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: