Akizungumza kutokea ndani ya Hifadhi ya Serengeti, ambapo amefanya ziara ya kushtukiza na kuuzunguka mpaka wote wa Mashariki ambapo hifadhi ya Serengeti inapakana na Pori Tengefu la Loliondo, lenye mgogoro wa muda mrefu, Dkt. Kigwangalla ameagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Maj. Gen. Gaudence Milanzi, kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Wanyama Pori, Prof. Alexander Songorwa mara moja. Ametoa sababu kuwa ni:

1. Tuhuma za kuhujumu Serikali kwa kutoa taarifa za siri za Serikali kwa vyombo vya habari na kutunga taarifa zenye kulenga kuchochea mgogoro wa Loliondo. (Jana usiku zilizunguka taarifa kwamba Dkt. Kigwangalla yupo na msafara wa gari mbili binafsi (private) njiani kwenda Loliondo na kwamba atalala Hotel ya Acacia iliyopo Karatu. Na leo msafara wake umekuwa ukifuatiliwa na watu wasiojulikana ambapo kila hatua aliyofikia ilikuwa ikiripotiwa kwenye mtandao, hali ambayo imetishia usalama wa kiongozi huyo).

2. Waziri Kigwangalla amesema Mkurugenzi huyo amekuwa akifanya kazi kwa maelekezo ya muwekezaji wa Kampuni ya Utalii wa Uwindaji ya OBC (maarufu kama kampuni ya kiwindaji ya wafalme wa Dubai). Kampuni hii imekuwa ikihusishwa na kashfa kwa miaka zaidi ya 26.

3. Aidha Prof. Songorwa amekuwa akihusishwa na kashfa ya kushiriki kugawa vitalu vya uwindaji kinyume cha sheria. Wiki mbili zilizopita Waziri Kigwangalla alisitisha mchakato wa kuhuisha leseni za uwindaji uliofanywa na Prof. Jumanne Maghembe, aliyekuwa waziri wa Maliasili na Utalii kwa tuhuma za rushwa na kukosekana uwazi kwenye mchakato huo. Pia ameelekeza mchakato wa kugawa vitalu sasa ufanywe kwa njia ya mnada.

Pia, ameelekeza TAKUKURU waanze kuchunguza kashfa za rushwa dhidi ya kampuni ya OBC na waanze kwa kumhoji bwana Mollel (Mkurugenzi wa OBC) ambaye amekuwa akijigamba kila kona kuwa alimhonga Maghembe dola 200,000, huyu kijana Kigwangalla dola 100,000 inamtosha! Dkt. Kigwangalla amesisitiza hahongeki na ndiyo maana jitihada za bwana Mollel kumuona zimekwama, na hata alipotumiwa ujumbe kupitia watu wake wa karibu alikataa.

Ili kuimarisha ulinzi wa mpaka wa Mashariki mwa Serengeti, Waziri Kigwangalla amewaondoa Askari wote wa Kituo cha Geti la Kleins kwa kuwa wamekuwa wakitumika na mwekezaji huyo ambaye ana mahusiano ya Karibu na Prof. Songorwa, na alikuwa na mahusiano ya karibu na Prof. Maghembe, Lazaro Nyalandu, balozi Kagasheki na Mawaziri wa Maliasili na Utalii wa zamani.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: