NASYEKZI  Lilash, mwanamke na mkazi wa Kijiji cha Arash, Tarafa ya Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro, Mkoani Arusha, amelazimika kumwachisha ziwa mtoto wake wa mwaka mmoja na miezi sita baada ya kufanyiwa vitendo vya ubakaji, anaandika Nasra Abdallah.
Akizungumza na mwandishi wetu, mwanamke huyo amesema vitendo hivyo alifanyiwa wakati wa operesheni ya kuwaondoa wafugaji, iliyofanyika kwa miezi mitatu mfululizo katika vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Serengeti, huku Arash kikiwa kimojawapo.
Pamoja na baadhi ya wanawake kulalama kufanyiwa hayo, aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alijitokeza mbele ya vyombo vya habari, na kusema kwamba katika operesheni hiyo hakuna kuku, mbwa wala binadamu waliojeruhiwa.
Nasyekzi amesema kumuachisha huko mtoto ziwa kumetokana na kutokuwa na uhakika kama amepata ujauzito au la na hivyo  anaogopa kumnyonyesha mtoto kwa kuwa kwa tamaduni za kabila lao sio vizuri unapokuwa na mimba uendelee kunyonyesha.
Pia ameongeza kuwa jambo hilo linamuumiza na ana wasiwasi mtoto wake anaweza asiwe na afya nzuri huko siku za usoni, kwa kuwa utamaduni wao ni kunyonyesha mtoto hadi anapofikisha umri wa miaka mitatu hadi mitatu na nusu.
“Tangu nilipofanyiwa ukatili huo na namna ninavyoona siku zangu nina wasiwasi huenda nimeshika mimba na ili kumuepushia mtoto asipatwe na matatizo nimeona ni vema nikamwachishwa,” amesema mama huyo  mwenye jumla ya watoto watatu.
Mbali na mtoto, pia Nasyekzi amesema kwa sasa hakutani na mume wake kimwili yapata miezi mitatu sasa tangu afanyiwe ukatili huo kwa kuwa bado anaugulia maumivu.
Akielezea namna alivyofanyiwa vitendo hivyo, ameeleza kwamba ilikuwa Oktoba 22 mwaka huu, askari waliokuwa wakifanya operesheni hiyo, walifika nyumbani kwake muda wa saa moja asubuhi na kumkuta akiwa amelala na walipoingia ndani walimtandika viboko na kumtaka atoke nje kisha kumburuza hadi porini na kuanza kumbaka.
Hata hivyo anasema watu hao akiwaona anawatambua, na kuiomba serikali kuhakikisha inawachukulia hatua askari wote waliohusika kuwabaka wanawake ambao mpaka leo siyo tu wameathirika kiafya bali hata kisaikolojia na kuwafanya waishi kwa aibu mbele ya jamii.
Operesheni ya kuwaondoa wafugaji katika Tarafa hiyo ya Loliondo ilianza Agosti 13, ambapo mbali na kukamatwa kwa mifugo yao pia kuliambata na kuchomewa maboma yao na kuwaacha wengi wakiwa hawana mahala pa kuishi na  kupoteza mali zenye thamani ya mamilioni.
Operesheni ondoa mifugo, iliyondana sambamba na  uchomaji wa maboma, ilifanywa na polisi wa Longido wakishirikiana na wale wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, (SENAPA) pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, (NCAA) huku vitongoji zaidi ya 14 vikiwa vimeathirika
Chanzo cha mgogoro huo kimetokana na Mamlaka hizo za Hifadhi, kutaka kumega eneo la kilometa 1500 katika vijiji hivyo na kupafanya rasmi pori tengefu litakalounganishwa na hifadhi  ya Taifa ya Serengeti.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: