Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amezitaka Taasisi zilizochini ya Wizara yake kuwajibika katika nafasi zao za uongozi na siyo kusubiria mpaka kiongozi wa juu aibue changamoto zinazojitokeza katika maeneo ya kazi
Waziri Ndalichako amesema kupitia kikao kazi hicho watendaji wataweza kujifunza na kubaini mapema viashiria ambavyo vitaonekana kukwamisha utekelezaji wa mipango ya wizara.
Amesema lengo la kikao hicho ni kuzuia madhara badala ya kusubiri madhara yatokee, hivyo kupitia kikao kazi hicho watendaji watajifunza kwa lengo la kufikia na kutekeleza malengo ya Wizara yaliyokusudiwa
Waziri Ndalichako pia amezitaka Taasisi na Watendaji wa Wizara hiyo kuanzia leo kuacha mara moja kulipana stahili ambazo hazifuati miongozo na nyaraka za serikali.
Profesa Ndalichako ametaja baadhi ya stahili ambazo zimekuwa zikilipwa bila kufuata taratibu na miongozo hiyo kuwa ni pamoja na posho za kujikimu, Nyumba, umeme na simu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amesema mkutano huo umelenga kuondoa viashiria hatarishi ambavyo vimekuwa vikikwamisha ufanisi katika utendaji kazi wa wizara.
Dkt. Akwilapo amewataka washiriki wa mkutano huo kuandaa mpango mkakati wa kuweza kutambua mapema viashiria hatarishi na kuvifanyia kazi ili kufikia malengo ya wizara.
Kikao kazi hicho ambacho kimeanza leo kitahusisha pia Wakurugenzi wasaidizi, waratibu wa miradi na wasaidizi wa miradi,wathibiti ubora na wakuu wa vitengo vya Wizara hiyo.
Imeandaliwa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Post A Comment: