WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji
Lindi (LUWASA), Mhandisi Adam Alexander (pichani mwenye mafaili) kwa
kosa la matumizi mabaya ya ofisi pamoja na kushindwa kusimamia ujenzi wa
kituo cha kuzalisha maji katika Manispaa ya Lindi.
Waziri
Mkuu amemkabidhi Mhandisi huyo kwa Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Lindi,
Bw. Stephen Chami na kumuelekeza afanye uchunguzi zaidi juu ya suala
hilo.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana Jumatano, Oktoba 19, 2016 wakati
alipotembelea mradi wa maji wa Ng'apa ambapo aliagiza nafasi hiyo
ikaimiwe na Mkurugenzi Msaidizi wa mamlaka hiyo, Mhandisi Idrisa
Sengulo.
"Kamanda
wa TAKUKURU fanya mapitio ya kina ya mshahara wake. Yeye anasema
analipwa Wizarani, mimi najua analipwa na LUWASA. Angalia kazi
aliyokwenda kuifanya Dar es Salaam kama inalingana na siku alizokaa,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Mhandisi
hiyo anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya fedha
za ofisi pamoja na kupokea mshahara bila la kulipa kodi ya mapato ya
mshahara (PAYE), kujilipa kiwango kikubwa cha posho pamoja na kusafiri
kwa muda mrefu.
Waziri
Mkuu alisema Serikali haiwezi kuvumilia kuona wananchi wanapata shida
huku watendaji waliopewa dhamana ya kuwatumikia hawaonekani kwenye vituo
vyao vya kazi. "Huyu nimemuita mimi aje huku, hadi jana alikuwa Dar es
Salaam."
Alipoulizwa
sababu za kutokuwepo ofisini kwake kwa muda mrefu, Mkurugenzi huyo
alisema kwamba alikuwa Dar es Salaam akiandika maombi ya fedha kwa ajili
ya kutatulia changamoto mbalimbali zinazoikabili mamlaka hiyo.
"Unatumia
siku ngapi kuandika proposal, msomi unatumia mwezi mzima kuandika
proposal na unakaa Dar es Salaam hata Katibu Mkuu wako hajui na huko
unajilipa posho tu! Tena badala ya kulipwa sh.120,000 kwa siku wewe
unajilipa sh.150,000. Hatuwezi kuvumilia hali hii,” amesema.
Waziri Mkuu amemaliza ziara yake siku tatu mkoani Lindi na amerejea jijini Dar es Salaam.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Post A Comment: