Tarehe 12.10.2016 majira ya saa 16:35 katika eneo la Busenga “A” kata ya Buswelu wilaya ya Ilemela jiji na mkoa wa Mwanza, askari walifanikiwa kumkamata mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Juma Biria miaka 42, mfanya biashara na mkazi wa mtaa wa Busenga akiwa na vifaa vya kutengeneza noti bandia ambavyo ni kemikali ikiwa ndani chupa kubwa, sabuni ya maji iliyowekwa ndani ya chupa ndogo, karatasi zilizokatwa mfano wa noti ya shilingi elfu kumi pamoja na unga ambao bado haujafahamika ni wa kitu gani, kitendo ambacho ni kinyume na sheria na taratibu za nchi .


Inadaiwa kuwa mtuhumiwa tajwa hapo juu akishirikiana na wenzake amekuwa akifanya shughuli hiyo ya uhalifu, ndipo zilipatikana taarifa za kiintelejensia kuhusiana na uhalifu huo, ndipo askari waliweza kufuatilia na kufanikiwa kumtia nguvuni mtuhumiwa huyo.


Aidha kwa sasa jeshi la polisi lipo katika mahojiano na mtuhumiwa, pindi uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani ili hatua  stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake. Aidha jitihada za kuwasaka wenzake wanaodaiwa kushirikiana na mtuhumiwa huyu katika uhalifu huo bado zinaendelea.


Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza naibu kamishina wa polisi Ahmed Msangi anatoa rai kwa wakazi wa jiji na mkoa wa Mwanza, akiwataka kushirikiana na jeshi la polisi katika kupambana na wahalifu wa aina kama hii, ili waweze kufikshwa katika vyombo vya sheria, kwani jeshi la polisi linaamini endapo wananchi wataendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi lao, tutaweza kukomesha uhalifu katika mkoa wetu.


imetolewa na:


DCP: Ahmed Msangi

Kamanda wa polisi (m) Mwanza

Share To:

msumbanews

Post A Comment: