Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akitoa maelekezo
kwa uongozi wa Wilaya ya Kibondo,alipotembelea ofisi hizo mkoani
Kigoma.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, akisikiliza
taarifa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Martin Mkisi mara
baada ya kutembelea ofisi hizo mkoani Kigoma.
Mkuu wa
Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali (Mstaafu), Emmanuel Maganga,
akikabidhi taarifa ya maendeleo ya miundombinu ya mkoa wake kwa Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, alipomtembelea
ofisini kwake.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, akikagua moja ya
vifaa vinavyotumika kupima aina ya udongo unaotumika kujengea barabara
katika maabara iliyopo kwenye kambi ya Mkandarasi anayejenga barabara ya
Kidahwe-Kasulu KM 50. Wa Pili Kulia ni Mhandisi wa Maabara kutoka
kampuni China Railway 15th Group Eng. Raphael Ndimbo.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akikata moja ya
nondo katika ujenzi wa Daraja la Muzye lililopo kwenye barabara ya
Kidahwe-Kasulu KM 50 wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara
hiyo.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (kushoto), akitoka
kukagua ujenzi wa daraja la Muzye lililopo kwenye barabara ya Kidahwe-
Kasulu KM 50 wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo. Wa
pili kushoto ni Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa
Kigoma Eng. Narcis Choma.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa agizo kwa
Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kushirikiana na Jeshi la Polisi
pamoja na wananchi kuwabaini na kuwachukulia hatua kali za kisheria
madereva wote wa malori ya mchanga na kokoto watakaobainika kutofuata
sheria za ubebaji wa bidhaa hiyo na hivyo kusababisha uharibifu wa
miundombinu ya barabara.
Waziri
Mbarawa ametoa agizo hilo mkoani Kigoma katika ziara yake ya kukagua
barabara ya Kidahwe-Kasulu yenye urefu wa kilometa 50 ambapo pamoja na
mambo mengine amesema Serikali inatumia fedha nyingi kujenga miundombinu
ya barabara kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla hivyo haita
mvumilia mtu yeyote atakayebainika kuharibu miundombu hiyo kwa makusudi.
“Kuanzia
sasa Serikali haitavumilia madereva wasiozingatia kanuni na sheria za
usafirishaji wa mizigo katika barabara nchini, hivyo nawaagiza Mameneja
wa TANROADS katika mikoa yote nchini kusimamia sheria ili kudhibiti
miundombinu ya barabara, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha,
Profesa Mbarawa ameliomba Jeshi la Polisi kushirikiana vema na
makandarasi wanaojenga miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali
nchini kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya watu wasio
waaminifu ambao wanaiba vifaa vya makandarasi jambo linalochangia
kukwamisha shughuli za ujenzi wa barabara.
Amewataka
wananchi wa Wilaya ya Kasulu kutoa ushirikiano kwa mkandarasi wa
kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation anayejenga barabara
hiyo ili kuwezesha ujenzi huo kukamilika haraka.
Naye
Meneja wa TANROADS mkoa wa Kigoma Eng. Narcis Choma, amebainisha
changamoto zinazokabili mradi huo kuwa ni wizi wa mafuta na vifaa vya
ujenzi hali inayosababisha mradi kusuasua.
“Wananachi
tambueni kuwa fedha hizi ni za kwenu mnapohujumu vifaa vya ujenzi ni
dhahiri mnajicheleweshea maendeleo na kukwamisha fursa za kiuchumi
katika wilaya yenu”, amesema Eng. Choma.
Kwa
upande wake Mhandisi Mkazi Mekbib Tesfaye anayesimamia mradi huo kutoka
Kampuni ya DOCH Limited, amesema kuwa mradi huo umefikia asilimia 24
ambapo kwa sasa kazi inayofanyika ni ujenzi wa madaraja mawili na
makalvati katika barabara hiyo.
Katika
hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa ametembelea Chuo cha Mamlaka ya
Hali ya Hewa Mkoani Kigoma na kuahidi uongozi kuwa atazishughulikia
haraka changamoto kadhaa zinazokikabili chuo hicho ili kuweka
mazingira rafiki ya kujisomea kwa wanafunzi wanaosomea taalauma hiyo.
“Nitahakikisha
chuo hiki kinajengewa mabweni ya wanafunzi pamoja na kuongeza gari kwa
ajili ya shughuli mbalimbali zinazofanyika hapa”, amefafanua Waziri
Mbarawa.
Kaimu
Mkuu wa Chuo hicho Peter Mlonganile wakati akisoma taaraifa ya chuo
hicho kwa Waziri huyo amesema kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto
hizo chuo hicho kinaendelea kutoa mafunzo hayo kwa viwango
vinavyotakiwa ikiwa ni pamoja na kuzitatua changamoto ndogo ndogo
zinazo kikabili chuo hicho.
Prof.
Mbarawa yuko katika ziara ya kukagua miundombinu ya barabara, reli,
uwanja wa ndege, katika mkoa wa Kigoma ikiwa ni mkakati wa Serikali wa
kuboresha miundombinu hiyo na kuuwezesha mkoa kufanya biashara kirahisi
na mikoa mingine ya Tanzania na nchi za Congo DRC, Rwanda na Burundi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Post A Comment: