Kikosi Maalumu cha Kupambana na Ujambazi wa Kutumia Silaha cha Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kilifanikiwa kukamata watuhumiwa wanne wa ujambazi waliohusika katika mauaji ya askari polisi 4 katika benki ya CRDB iliyopo maeneo ya Mbande, Mbagala jijini Dar es Salaam.

Kamishna wa Kanda hiyo, Kamanda Simon Sirro wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, amesema watuhumiwa hao walikamatwa wakati wa majibizano ya risasi yaliyotokea Oktoba 11, 2016 katika pori la Dondwe lililopo Chanika.

“Kikosi kilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja, baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa ni jambazi na ndiye aliyehusika katika mauaji ya askari polisi huko Mbande,” amesema.

Kamanda Sirro ameongeza kuwa “Baada ya kumkamata mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na tukio hilo akiwa na wenzie saba, alitupeleka mahala walipo wenzake, ila alikimbia, wenzie walipojua polisi wapo maeneo hayo, walianza kurusha risasi ndipo polisi nao wakaanza kurusha risasi.”

Kamanda Sirro amesema kuwa, watuhumiwa hao walizidiwa na mashambulizi ya risasi ambapo walijeruhiwa vibaya na kwamba walifariki dunia wakiwa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Amesema askari polisi walifanikiwa kuipata bunduki ya kijeshi aina ya SMG iliyofutwa usajili ambayo watuhumiwa hao waliipora kutoka mikononi mwa polisi waliowaua mbande ikiwa na risasi 22 ndani ya magazine.

Katika tukio lingine, Kamanda Sirro amesema mnamo Oktoba 11, 2016 maeneo ya magomeni polisi wakiwa doria walifanikiwa kukamata bastola moja aina ya bereta baada ya kutelekezwa na kundi la vijana.

Pia amesema Jeshi la Polisi limekamata watuhumiwa watatu wakiwa na bomu moja la kienyeji, mapanga manne, visu viwili, na bisibisi moja.

Vilevile Jeshi la Polisi Dar es Salaam Oktoba 12, 2016 walikamata panya road zaidi ya 10 maeneo ya Mbagala.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: