MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu imewasomea maelezo ya awali (PH) washtakiwa
wanane wakiwamo, wabunge watatu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo(Chadema) katika kesi ya kumpiga na kumjeruhi Katibu Tawala wa
Mkoa wa Dar es Salaam(RAS),Theresia Mmbando.
Akisoma
maelezo hayo mbele ya Hakimu, Huruma Shaidi, Wakili wa Jamhuri, Frola
Massawe aliwataja washtakiwa hao kuwa ni pamoja na Halima Mdee (Kawe),
Mwita Waitara (Ukonga), Saed Kubenea (Ubungo), aliyekuwa Diwani wa Kata
ya Saranga, Ephreim Kinyafu, Diwani wa Kata ya Kimanga, Manase Njema na
mfanyabiashara Rafii Juma.
Wakili
Massawe alidai mahakamani hapo kuwa, washtakiwa hao kwa pamoja
wanadaiwa kutenda kosa hilo Februari 27, mwaka huu katika ukumbi wa
Karimjee, ulioko wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam ambako kulikuwa na
uchaguzi wa meya na msadizi wake.
Alidai
kuwa,katika ukumbi huo,kulitolewa taarifa ya kutokuwepo kwa uchaguzi
huo kutokana na kuwepo kwa zuio kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
ambapo liliwataka kutofanya uchaguzi huo mpaka zuio hilo
litakapomalizika ndipo uchaguzi ufanyike.
Alidai
kuwa, mshtakiwa wa kwanza ambaye si mbunge (Rafii Juma), hakuridhishwa
na taarifa hiyo ndipo aliposhirikiana na washtakiwa wengine kwa
kumvamia, kumpiga na kumchania nguo RAS Mmbando hali iliyosababishia
majeraha.
Alidai,
baada ya kutokea kwa vurugu hizo, polisi waliingilia kati na kumuuliza
kama aliweza kuwafahamu waliompiga, baada ya kuulizwa hivyo, alidai
kumfahamu mshtakiwa wa pili, ambaye ni Halima Mdee.
Alidai
kuwa, baada ya hapo, polisi walilazimika kuchukua daftari la mahudhurio
ya siku hiyo na kuanza kuita majina mmoja baada ya mwingine na kupiga
gwaride la utambulisho ambalo lilimsaidia kuwatambua washtakiwa wote na
kukamatwa na kuwafikisha polisi na mahakamani.
Baada ya kusomewa maelezo hayo, washtakiwa hao walikubali taarifa zao binafsi lakini walikana shtaka linalowakabili.
Hata hivyo, upande wa mashtaka ulidai kuleta mashaidi 16 ambao watatoa ushaidi kwenye kesi hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Shaidi alihairisha kesi hiyo hadi Novemba 14 mwaka huu kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushaidi.
Post A Comment: