WAZIRI
wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage ametoa siku nne kwa
wafanyabiashara waliopitisha makontena 100 bandarini bila kukaguliwa na
Shirika la Viwango Tanzania (TBS), wakatoe taarifa katika shirika.
Mwijage
alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na
waandishi wa habari baada ya kupata taarifa kuwepo kwa makontena 100,
yaliyotolewa bandarini kwa siku zilizopita bila kukaguliwa na TBS.
“Nawataka
wafanyabiashara wote waliochukua kontena hizo, wajisalimishe haraka TBS
kabla ya kufika Jumanne ili wakaguliwe. Najua kuanzia kesho (leo) ni
mapumziko, lakini TBS itaweka dawati la kuwasikiliza mpaka Jumatatu na
ikifika Jumanne hatua zitachukuliwa kwa wahusika wote,” amesema Mwijage.
Alisema
wafanyabiashara ambao hawatajisalimisha baada ya kumalizika kwa siku
hizo, hatua stahiki zitachukuliwa ikiwemo kulipa faini ya asilimia 15.
Aidha,
alisema kwa mawakala wa forodha wote, waliohusika kutoa kontena hizo
wizara yake itawasiliana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango
ili kuona hatua za kuchukua kwa kuwa serikali haiwezi kukubali mchezo
huo.
“Tayari
tulishafunga michezo ya namna hii na tumeanza maisha mapya kwa hiyo
mawakala na wote mliohusika kutoa kontena hizo sababu hazijafika mbali
tunaomba mtueleze zilipo ili tukazikague,” aliongeza.
Pia
alisema kontena hizo zilipaswa kukaguliwa na TBS, lakini baada ya tukio
hilo kontena hizo zitakaguliwa na shirika hilo wakishirikiana na Tume
ya Ushindani Tanzania (FCC).
Aidha,
amewaagiza TBS na FCC wafuatilie watu wao na kuziona bidhaa hizo, kwani
watakaoshindwa hawatapewa cheti cha ubora bila kuona bidhaa na
kukaguliwa.
“Sisi
hatutaki mje mtueleze ni mzigo kiasi gani ili tupige penati hapana
tunataka hilo kontena mlione na hiyo bidhaa muione na mkague,” aliongeza waziri huyo.
Kwa
upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Egid Mubofu alisema ni
vyema wafanyabiashara hao wakafuata maagizo hayo na kujitokeza
kukaguliwa ilikuepuka faini hiyo ya asilimia 15.
Alisema
upitishaji wa bidhaa bila kukaguliwa na shirika hilo unaweza kuleta
madhara makubwa kwa watumiaji ambao hawajui kama bidhaa yako imekaguliwa
ubora.
“Najua
wafanyabiashara wengine watasema hatuendi kukaguliwa sababu hataitumia
bidhaa hiyo, lakini anasahau kama anaweza siku moja na yeye akatumia
bidhaa hiyo ambayo haijakaguliwa ni vyema wakawa wazalendo na kufuata
maagizo waliyopewa,” alisema Mubofu.
TBS
imeanzisha utaratibu mpya wa kulipisha faini mizigo inayoingia hapa
nchini, ambayo haikukaguliwa wakati iko nchini China. Faini ni asilimia
15 ya thamani ya mzigo ulioingia.
Post A Comment: