Vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge vitaanza tarehe 17 Oktoba hadi tarehe 30 Oktoba 2016, Mjini Dodoma kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Tano wa Bunge uliopangwa kuanza tarehe 1 Novemba 2016. Kufuatia Ratiba hiyo ya shughuli za Kamati, Waheshimiwa Wabunge wote wanapaswa kuwa wamewasili Mjini Dodoma ifikapo Jumapili tarehe 16 Oktoba, 2016 kwa ajili ya kushiriki vikao hivyo.
 
Katika Vikao hivyo, shughuli zilizopangwa kutekelezwa na Kamati ni kama ifuatavyo:
  1. a) KUPOKEA MAONI YA WADAU WA MISWADA MBALIMBALI
Kamati mbili (2) za Kisekta zitajadili Miswada miwili ya Sheria ambapo Kamati ya Katiba na Sheria itajadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, Na. 3 wa Mwaka 2016 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2016] na itakuwa na vikao vya kupokea maoni ya wadau kuhusu Muswada huo siku ya tarehe 21 Oktoba, 2016 katika Ukumbi wa Serengeti, Ofisi ya Hazina Mjini Dodoma kuanzia saa tano (5:00) Asubuhi ambapo Sheria hiyo ina jumla ya Sheria 9 zitakazofanyiwa marekebisho na Muswada huu.
 
Kamati nyingine ni Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ambayo itajadili Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa Mwaka 2016 [The Media Services Bill, 2016] na itakuwa na vikao vya kupokea maoni ya wadau kuhusu Muswada huo siku ya tarehe 19 Oktoba, 2016 Katika ukumbi ulipo katikaJengo la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Mjini Dodoma kuanzia saa tatu kamili (3:00) asubuhi hadi saa Tisa(9:000) Alasiri.
 
Pamoja na kamati hizo mbili za kisekta, pia Kamati ya Sekta Mtambuka ambayo ni Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo nayo imepanga kufanya mikutano ya kusikiliza maoni ya wadau (Public Hearing)kuhusiana na Sheria Ndogo zilizowasilishwa na Serikali katika Mkutano wa Nne wa Bunge. Mikutano hiyo inatarajiwa kufanyika kati ya Jumanne tarehe 18 Oktoba, 2016 na Alhamisi tarehe 27 Oktoba, 2016 katika Jengo la Hazina (Treasury Square) Mjini Dodoma.
 
Wadau wote katika Miswada tajwa hapo juu wanakaribishwa kufika mbele ya Kamati kutoa maoni yao katika tarehe na muda uliotajwa.
  1. b) KUPOKEA TAARIFA ZA KIUTENDAJI WA WIZARA
Kamati tisa (9) za kisekta zitapokea Taarifa za utendaji wa Wizara zinazosimamiwa na Kamati hizo kwa mujibu wa Kifungu cha 7 (1) (c) na (d) cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo Januari, 2016.
  1. i) Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama itapokea na kujadili Taarifa za wawakilishi wa Bunge katika SADC – PF, ACP – EU na CPA kwa mujibu wa Kifungu cha 7 (2) (iii) na (iv) cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016.
  2. ii) Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa itafanya ziara mbili Mkoani Dodoma kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Wizara inazozisimamia kwa mujibu wa Kifungu cha 7 (1) (d) cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge
iii) Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) itapokea na kujadili Taarifa za Uwekezaji unaofanywa na Mashirika/Taasisi za Umma tisa (9).
  1. c) UCHAMBUZI WA TAARIFA KUHUSU HESABU ZILIZOKAGULIWA
Kamati mbili za usimamzi wa Fedha za Umma zitafanya uchambuzi wa taarifa kuhusu Hesabu zilizokaguliwa kwa Mwaka unaoishia tarehe 30 Juni, 2015 ambapo Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) itachambua taarifa kuhusu Hesabu zilizokaguliwa kwa Mwaka unaoishia tarehe 30 Juni, 2015. Katika kipindi hicho, jumla ya Mashirika/Taasisi tisa (9) na Maafisa Masuuli wa Mafungu (Votes) tatu (3) watakutana na Kamati kwa madhumuni hayo.
 
Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) itachambua Hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2015, na Katika kipindi hicho, Hesabu za Halmashauri kumi na sita (16) zitajadiliwa.
 
Ratiba zote za Shughuli za Kamati za Bunge pamoja na Miswada itakayoshughulikiwa na Kamati katika kipindi hiki inapatikana kupitia tovuti hii ya Bunge.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: