Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala imekataa mapendekezo ya kufanyia marekebisho Sheria ya Leseni za Uchukuzi ya mwaka 1973 yenye lengo la kuongeza kiwango cha adhabu ya faini hadi kufikia asilimia 500 kwa watakaokiuka masharti ya leseni hizo.
Mapendekezo hayo yaliwasilishwa mbele ya kamati hiyo mjini Dodoma jana na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra).
Baada
ya kuyakataa mapendekezo hayo, kamati hiyo imetoa muda wa siku mbili
kwa Sumatra kuhakikisha inawasilisha mbele ya kamati hiyo mapendekezo
yanayokubalika.
Sumatra
inapendekeza kuongeza kiwango cha adhabu ya faini kutoka kati ya Sh
10,000 na Sh 50,000 hadi Sh 200,000 na 500,000 kwa watoa huduma za
uchukuzi, watakaokiuka masharti ya leseni zao.
Mwenyekiti
wa kamati hiyo, Mohammed Mchengerwa alisema mapendekezo hayo, yatazidi
kuwaongezea mzigo Watanzania badala ya kuwasaidia.
Alisema
kiwango hicho cha faini kubwa, kamwe hakitazuia tatizo la ajali za
barabarani, zaidi ya kuongeza ukubwa wa tatizo la rushwa.
“Serikali
ya Awamu ya Tano imejipanga kuwasaidia wananchi, lakini mapendekezo
haya yatazidi kuwaongezea mzigo kwa sababu kiwango cha faini hizi kama
kitapitishwa, watoa huduma za uchukuzi watahamishia hasara yao kwa
wananchi,” alisisitiza.
Aliitaka
mamlaka hiyo, kwenda kuyafanyia kazi tena mapendekezo hayo kwa
kuwasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuwasilisha viwango vya
faini vinavyokubalika.
Mmoja
wa wajumbe wa kamati hiyo, Joseph Mhagama ambaye pia ni mbunge wa
Madaba, alisema mapendekezo hayo hayana nyongeza yoyote, itakayoisaidia
serikali katika kudhibiti tatizo la ajali barabarani.
“Kwa
sasa serikali imeweka nguvu zake katika kupunguza ajali za barabarani,
lakini kiwango cha faini hizi hakina uhusiano wowote na jitihada hizi
zaidi ya kuiongezea Sumatra mapato na kuwapa mzigo walipa kodi,” alisema.
Akiwasilisha
mapendekezo ya mamlaka hiyo mbele ya Kamati hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa
Sumatra, Gilliard Ngewe alisema mapendekezo ya marekebisho ya sheria
hiyo, yamelenga kuiboresha zaidi sheria hiyo ya leseni za uchukuzi.
Alisema
marekebisho hayo, pia yatasaidia mamlaka hizo kuendana na mahitaji ya
sasa hasa katika eneo la adhabu ya faini, hali itakayopunguza kiwango
kikubwa cha kukiukwa kwa masharti ya leseni hizo za uchukuzi.
Post A Comment: