Polisi na raia wanne wamejeruhiwa kwa bomu la kutupwa kwa mkono walipokuwa wakimkamata mtuhumiwa wa ujambazi kwenye Kijiji cha Uvinza mkoani Kigoma. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Ferdinand Mtui alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Oktoba 14. 

Alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Yahya Kamuhanda (49) mkazi wa kijiji hicho. Mtui aliwataja majeruhi hao kuwa ni askari polisi F.3187 Koplo Isaya na raia Saidi Mohamed, Seleman Kashali, Joseph Daudi na Hassan Nasibu, wote wakazi wa Kijiji cha Uvinza. 

Alisema askari walipata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba Kamuhanda anajiandaa kufanya uhalifu hivyo waliweka mtego eneo la Uvinza Madukani alikokwenda kununua mahitaji. 

Alidai kuwa alipotambua anafuatiliwa alitupa bomu ndipo polisi walimpiga risasi mguuni na wananchi walimvamia na kumshambulia kabla ya askari kutumia nguvu kumwokoa asiuawe kwa kipigo. 

Mtui alisema mtuhumiwa alipohojiwa alisema alificha bunduki kijijini kwao Lukole wilayani Ngara mkoani Kagera, ambako askari walikamata SMG yenye namba 78GA5062 ikiwa imefukiwa ardhini.

 Pia, walikamata magazini saba, moja ilikuwa na risasi 40, nne (risasi 30 kila moja) na mbili (risasi 20 kila moja) na risasi 75 zilikuwa kwenye mfuko wa sandarusi. Pingu moja na funguo zake, maski tisa na laini 20 za mtandao wa Halotel ambazo hazijasajiliwa. 

Mtui alisema mtuhumiwa huyo alifariki dunia juzi akipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma (Maweni). Alisema majeruhi wote watano walipata matibabu hospitalini hapo na waliruhusiwa kurudi nyumbani. 

Source P.T

Share To:

msumbanews

Post A Comment: