SERIKALI
ya Japan, kupitia Shirika lake la Maendeleo-JICA, imeahidi kuongeza
kiwango cha ruzuku kwa serikali ya Tanzania ili kufadhili miradi
mbalimbali ikiwemo kilimo, Maji, miundombinu ya barabara na huduma
nyingine za jamii ili kuisaidia kufikia maendeleo yaliyokusudiwa kwa
wananchi wake.
Ahadi
hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Japan-JICA,
Hiroshi (Hiro) Kato, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa
Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Jijini Washington DC, nchini
Marekani.
“Kabla ya
mwaka 2013 tulikuwa tunatoa ruzuku ya dola milioni 1 kwa Tanzania kila
mwaka, lakini kuanzia mwaka 2013 tumeongeza kiwango hadi kufikia dola
milioni mia 3 kila mwaka na tunatarajia kuongeza kiwango hicho siku za
hivi karibuni” aliongeza Makamu huyo wa Rais wa JICA
Kato
amesema kuwa Tanzania na Japan ni marafiki wa muda mrefu na kwamba nchi
hiyo itaendelea kuisaidia kwa kutekeleza miradi mbalimbali yenye kuleta
tija kwa uchumi wa nchi na maisha ya watanzania kwa ujumla.
“Hivi
sasa tunataka kuanza kutekeleza awamu nyingine ya mradi wa kilimo cha
umwagiliaji cha zao la mpunga ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo ambalo
ni muhimu sana” Aliongeza Kato.
Amesema
kuwa Japan pia imeamua kuongeza kiwango cha ufadhili kwa Bara la Afrila
kutoka Dola Milioni 13 ambazo nchi hiyo ilikuwa ikitoa kwa kipindi cha
miaka mitano kuanzia mwaka 2013 hadi kufikia dola elfu 30 kwa mwaka
kuanzia mwezi Agosti, 2016 kwa kipindi cha miaka 3 ijayo.
Amesema
pia kuwa ili kuwajengea uwezo na ujuzi vijana wa kiafrika, Japan
imeanzisha program ya kutoa elimu ambapo hivi sasa vijana 60 kutoka nchi
mbalimbali za kiafrika wamepelekwa nchini humo kujifunza kwenye vyuo
vilivyoko huko na watapelekwa kwenye kampuni na mashamba makubwa
yanayojihusisha na kilimo ili waweze kupata uzoefu na kuwa chachu ya
mabadiliko watakaporejea katika nchi zao.
Akiongea
na Makamu huyo wa Rais wa Shirila la Maendleo la Japan-JICA, Waziri wa
Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameishukuru Japan kwa kuisaidia
Tanzania katika Nyanja mbalimbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Ametaja
baadhi ya miradi ambayo nchi hiyo inafadhili nchini Tanzania kuwa ni
ujenzi wa barabara ya Arusha hadi Holili hadi Taveta nchini Kenya,
Ujenzi wa barabara ya Juu (Flyover) ulioanza eneo la Tazara ili
kupunguza msongamano Jijini Dar es salaam, miradi ya maji na kilimo cha
umwagiliaji.
“Asilimia
75 ya wananchi wetu wanategemea kilimo kwahiyo uamuzi wa Japan wa
kuwekeza fedha nyingi kwenye miradi ya kilimo cha umwagiliaji ni jambo
tunalolipongeza kwasababu kilimo kitakuwa na tija na kitaendeshwa
kibiashara” Alisema Dkt. Mpango.
Ameishukuru
pia serikali ya Japan kwa kufanya utafiti na upembuzi yakinifu wa mradi
wa kudhibiti mafuriko ya mto Kondoa, eneo la mkoa wa Morogoro ili
kudhibiti mto huo usiharibu miundombinu ya reli ya kati.
“Mradi
huu ni muhimu sana kwasababu serikali imekuwa ikiingia hasara karibu
kila mwaka kukarabati njia hiyo ya reli baada ya kusombwa na maji, hivyo
tunaishukuru Japan kwa kutusaidia kufanya utafiti huo ambao utasaidia
kukabiliana na hali hiyo” aliongeza Dkt. Mpango
Ameahidi
kuwa serikali ya awamu ya tano imejipanga kukusanya kodi na kuziba
mianya ya upotevu wa fedha za serikali ikiwemo kuanzisha mahakama
maalumu ya kushughulika na mafisadi ili kuleta nidhamu katika utumishi
wa umma.
Post A Comment: