Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama ametoa siku saba kwa taasisi za serikali, wizara, kampuni na watu binafsi kuhakikisha wanalipa madeni wanayodaiwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Waziri Mhagama pia ameziagiza bodi za wadhamini za mifuko mingine ya hifadhi ya jamii, kuhakikisha zinawashinikiza wadeni wao kulipa madeni yote wanayodaiwa ili kuiwezesha mifuko hiyo kujiendesha kwa ufanisi zaidi.

Ametoa tamko hilo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, alipotembelea miradi ya nyumba za NSSF iliyopo wilayani Kigamboni mkoani Dar es Salaam.

Amemtaka Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Erick Shitindi kuhakikisha uongozi wa mifuko unampatia ripoti ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika wote walioshindwa kulipa madeni yao kwa mifuko yao.

“Ninafahamu fika kuna mikataba ambayo ilisainiwa na pande zote mbili kabla ya kutolewa kwa hiyo mikopo na makubaliano mengine hivyo naomba basi mikataba hiyo itumike kufanikisha agizo hili,’’ alisema.

Pia alimuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa NSSF, Profesa Samwel Wangwe kuhakikisha anampatia ripoti muafaka ya utekelezaji wa agizo hilo.

“Kwa niaba ya serikali, ninataka kuona kwamba wadaiwa wote wa mifuko hii bila kujali nafasi zao kiuchumi au kisiasa wanalipa madeni wanayodaiwa…hii lazima ijumuishe kampuni, wawekezaji na taasisi za serikali,’’ alisisitiza.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara alisema licha ya mfuko wake kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo majengo, bado wateja wake wengi hawajalipa madeni wanayodaiwa na mfuko huo ikiwemo watu binafsi, taasisi za serikali na binafsi wakiwemo pia wale walionunua nyumba za shirika hilo.

Alisema shirika hilo, bado linadai Sh bilioni 20 kutoka kwa wapangaji wake, deni linalohusisha pia dola za Marekani milioni 1.2.

Alifafanua kuwa kiasi kingine cha Sh bilioni 86, kinadaiwa kama adhabu kutoka kwa waajiri walioshindwa kukamilisha makato ya wafanyakazi wao.

Madeni mengine ni pamoja na deni la Sh milioni 42 na dola za Marekani milioni 35.9 zilizotolewa kama mikopo kwa sekta binafsi mbalimbali huku mkopo mwingine wa Sh bilioni 38 ulitolewa kupitia Saccs na bado hazijarejeshwa.

“Hata hivyo, tumeanza kuchukua hatua mahsusi kulingana na matakwa ya sheria kuhakikisha kwamba madeni yote yanalipwa,’’ alibainisha Profesa Kahyarara.
 Waziri nchi ofisi ya waziri mkuu sera, uratibu, bunge ,vijana na watu wenye ulemavu  Mhe. Jenister Mhagama akiwa ameambatana na uongozi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) alipotembelea miradi ya nyumba za NSSF iliyopo wilayani Kigamboni mwishoni mwa wiki.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa NSSF Prof Samwel Wangwe. (kushoto) akizungumza mbele ya Waziri nchi ofisi ya waziri mkuu sera, uratibu, bunge ,vijana na watu wenye ulemavu  Mhe. Jenister Mhagama wakati waziri huyo alipotembelea miradi ya nyumba za NSSF iliyopo wilayani Kigamboni mwishoni mwa wiki. Wengine ni pamoja na Mkurugenzi mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara (kulia
 Mkurugenzi mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara (kulia) akizungumza mbele ya Waziri nchi ofisi ya waziri mkuu sera, uratibu, bunge ,vijana na watu wenye ulemavu Mhe.  Jenister Mhagama wakati waziri huyo alipotembelea miradi ya nyumba za NSSF iliyopo wilayani Kigamboni mwishoni mwa wiki. Wengine ni pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa NSSF Prof Samwel Wangwe (kushoto).
Share To:

msumbanews

Post A Comment: