Katibu Mkuu wa UVCCM Shaka Hamdu Shaka akiwa anaongea na wajumbe waliouthuria mkutano huo

Na LIDIA KISHIA ,Arusha

UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi, UVCCM, taifa itatuma mkaguzi wa hesabu na mali za jumuia hiyo mkoa wa Arusha, katika kipindi cha wiki mbili kuanzia Septemba 27 mwaka huu ili kupata ukweli zilipo shilingi milioni 112.8 za umoja huo zinazokusanywa kila mwaka kutokana na kodi ya maduka.

Makamu mwenyekiti UVCCM, Taifa, Mboni Mhita, aliyasema hayo jana mara baada ya kikao na wajumbe wa baraza la UVCCM ,mkoa wa Arusha, kilichofanyika ukumbi wa ccm ,mkoa na baada ya muda huo kamati ya taifa ya UVCCM, itarejea mkoani Arusha kufanyia kazi yaliyobainishwa na mkaguzi wa hesabu.

Mhita,ambae anaongoza kamati ndogo ya watu watatu ya UVCCM,taifa,alisema anawashangaa wajumbe wa baraza hilo kushindwa kuchukua hatua na kusimamia jumuia hiyo hadi washikane mashati wakati wao wakiwepo na sasa wanagombea vibanda vya maduka ambavyo hawakuvijenga na wala hawajajenga vipya.

Mhita, alisema baadhi ya wajumbe wa baraza la UVCCM, Mkoa wa Arusha, hawaelewi maana ya UVCCM, majukumu yao kwa kuwa hawajasoma kanuni za umoja huo na wameingia kwenye uongozi bila kuwa na sifa na ndio chanzo cha migogoro.

Wajumbe hao walikutana na UVCCM kwenye mchakato wa kugombea uongozi na hawajosoma kanuni na katiba ya UVCCM hivyo kuwepo mitafaruku ndani ya umoja huo mkoani Arusha, ambayo inakwamisha maendeleo na ufanisi wa shughuli za umoja huo.

Alibanisha kuwa baraza lazima libebe lawama kwa kushindwa kusimamia majukumu kutokana na kushindwa kuendana na sera za ccm kutokana na kukosa uadilifui, na kutokutambua majukumu yao

Kamati hiyo ndogo inafuatilia mgogoro wa UVCCM ,mkoa wa Arusha, ambapo miongoni mwa majukumu ya
kamati hiyo ni kuwasikiliza wajumbe wa baraza hilo kutokana na mgogoro uliojitokeza hivi karibuni.

Mhita, alilitaja jukumu lingine la kamati hiyo ndogo kuwa ni kupatiwa nyaraka za mikataba ya wapangaji wa maduka yote ya UVCCM, mkoa huo.

Aidha alisema kuwa baadhi ya viongozi wa baraza hilo waliandika barua ya kuwatukana na kuwadharirisha
viongozi wa UVCCM taifa lakini leo walipoulizwa kwenye kikao hicho wamekana saini zao.

Kwa upande wake Naibu katibu mkuu wa UVCCM taifa, Shaka Hamdu Shaka, alisema UVCCM ni taasisi
kubwa ya Chama cha Mapinduzi hivyo lazima wazingatie heshima, umoja na ushirikiano kwa kuwa ndizo nguzo za uvccm.

Amewaambia kuwa UVCCM, Inaongozwa na kanuni, mbili za Utumishi na Utawala ,taratibu za fedha , maadili ya viongozi .

Alisema kilichotokea kwenye uongozi wa UVCCM, mkoa wa Arusha ni kutokufuatwa kwa kanuni ,taratibu na
miongozo ya jumuia hiyo.

Alibainisha kuwa ukiukwaji huo wa kanuni kumesababisha mgogoro wa uongozi uliopelekea aliyekuwa mwenyekiti wake, Lengai kusimamishwa uongozi huku aliyekuwa katibu wa mkoa Ezakiel Mollel, nae akiondolewa kutokana na kukaidi maelekezo ya mwajiri wake kuhamia makao makuu.

Alisema kuwa anashangazwa kuona UVCCM ikiwa na wajumbe 16 wa kamati ya miradi jambo ambalo ni kinyume na kanuni za UVCCM kwa kuwa hakuna kifungu kinachoelekeza kamati iwe na wajumbe wengi kiasi hicho hata taifa haipo.

Aidha alisema UVCCM mkoa wa Arusha, inakusanya shilingi milioni 112.8 kwa mwaka makusanyo yanayotokana na maduka yaliyopo kwenye jengo la UVCCM mkoa lakini hazijulikani ziliko.

Awali mjumbe wa kamati hiyo kutoka mkoa wa Lindi,Amir Mohamed,aliwataka wanachama wa UVCCM mkoa wa Arusha, kujenga umoja na,upendo na kuacha kushughulikiana wao kwa wao na kusababisha migawanyiko ili kuiwezesha jumuia hiyo iweze kufikia malengo na kutimiza majukumu yake ya kisiasa.

Mohamed, alikuwa akitoa salamu za UVCCM taifa, kwenye kikao maalumu cha baraza la umoja wa Vijana mkoa wa arusha, iliyofanyika ukumbi wa CCM, Mkoa kilichokuwa kikisikiliza mgogoro wa uongozi wa jumuia hiyo.

Alisema UVCCM ni tanuru la kuoka viongozi na wajumbe wote wa baraza hilo wana wajibu kufahamu mipaka na misingi ya uongozi.

Alisema UVCCM,haitawavumilia watakaokiuka misingi na maadili itawatimua hivyo lazima watumie rasimilami za umoja huo walinde zingine kwa manufaa kwa kuwa UVCCM ni walinzi wa mali za chama na viongozi wake

Share To:

msumbanews

Post A Comment: